Njia Mpya ya Ufisadi Yabainishwa

Njia Mpya ya Ufisadi Yabainishwa
Mchambuzi wa masuala ya kisiasa nchini Tanzania, Michael Bante amemuomba Rais John Magufuli kurudisha mchakato wa Katiba ili kusudi waweze kubadilisha sheria ya wabunge na madiwani wanaojiuzulu, watumie gharama zao wenyewe kwa kuwa wanachokifanya sasa ni moja ya njia ya ufisadi.

Bante ametoa mapendekezo hayo wakati alipokuwa anazungumza kwenye mahojiano maalum na www.eatv.tv na kusema kwamba serikali inapaswa kuwekea makazo kwenye Katiba kusudi, kupunguza matumizi mabaya ya fedha katika kurudia uchaguzi mdogo kutokana na wabunge na madiwani kujiuzulu, na badala yake kutumia fedha hizo kwenye shughuli za kimaendeleo.

"Inapaswa tufike mahali turudi kwenye Katiba ili tuweke misingi mizuri, mtu anapotangaza nia ya kujiuzulu ubunge wake au udiwani kwa matakwa yake binafsi, basi kwanza aweke fedha itakayowezesha kufanyika uchaguzi wa marudio katika jimbo ambalo atakuwa anang'atuka. Maana serikali inatumia pesa nyingi kufanya uchaguzi wa marudio badala ya pesa hizo kuzitumia katika kufanyia masuala ya kimaendeleo", amesema Bante.

Mbali na hilo, Bante amemshauri Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt. John Magufuli kutoangalia upande mmoja tu wa kupokea wanachama wapya bali pia anapaswa kutaama na umasikini waliokuwa nao watanzania.

"Unaposema umeacha Ubunge maana hutaki kufanya kazi. Sisi kama wachambuzi tunasema kabisa mtu akitangaza kuacha Ubunge basi alipe gharama zote za uchaguzi lasivyo asijiuzulu. Rais Magufuli asiangalie tu kwa vile watu wanaingia kwenye chama chake anapaswa kuangalia umasikini wetu tuliokuwa nao watanzania...

Huu ni ufisadi mpya, Mbunge anaachia jimbo lake halafu serikali inaingia kwenye gharama nyingine nyingi na kupoteza muda wa wananchi wa kuacha kuendelea kufanya kazi zao na kuenda kujipanga kwenye viwanja kupiga kura tena", amesisitiza Bante.

Kauli hiyo ya Michael Bante imekuja muda mchache baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kutangaza tarehe rasmi ya uchaguzi mdogo wa marudio wa Ubunge katika majimbo matatu na wa udiwani katika kata mbili za Tanzania bara utakaofanyika Septemba 16, mwaka huu.

Majimbo hayo ni Korogwe vijijini, Mkoa wa Tanga kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo Stephen Hilary Ngonyani, Jimbo la Ukonga katika mkoa wa Dar es Salaam na Jimbo la Monduli mkoani Arusha baada ya waliokuwa wabunge wa majimbo hayo kujiuzulu uanachama wa vyama vyao na kukosa sifa za kusalia kuwa wabunge.

Kwa kipindi cha takribani miaka mitatu tayari wabunge watano wameshajivua nyadhifa zao, ambapo dimba lilifunguliwa na Lazaro Nyalandu kutoka CCM kwenda CHADEMA, Maulid Mtulia CUF kuelekea CCM, Godwin Mollel CHADEMA kwenda CCM, Waitara kutoka CHADEMA kurudi CCM pamoja na Julius Kalanga kutoka CHADEMA kurudi CCM.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad