Mchezaji wa zamani wa klabu ya Arsenal na timu ya taifa ya Nigeria, Nwanko Kanu ameitupia dongo zito klabu hiyo kuelekea msimu mpya wa mashindano ya ligi kuu nchini Uingereza (EPL) unaotarajia kuanza Agosti 11.
Arsenal ambayo imemuajiri kocha mpya, Unai Emery mwanzoni mwa mwezi juni baada ya kocha Arsene Wenger aliyedumu kwa miaka 22 klabuni hapo kuondoka.
"Kama itatokea Arsenal kushinda taji la EPL basi itakuwa ni maajabu ". Amesema Nwanko.
"Kwa kocha mpya, Unai Emery itakuwa ni changamoto kubwa kwake msimu huu, kwakuwa mashabiki wanataka kocha ashinde ubingwa katika msimu wake wa kwanza jambo ambalo ni ngumu kwake". Ameongeza nguli huyo wa soka.
Klabu ya Arsenal imesajili wachezji watano mpaka sasa ambao, Kanu anaamini wanahitaji muda zaidi wa kuzoea mazingira ya klabu hiyo pamoja na kuelewa mfumo wa kiuchezaji wa kocha, akitaja kuwa usajili huo ni mzuri kwa mbinu za kiulinzi kuliko kuzalisha magoli kitu ambacho kinahitajika zaidi katika klabu.
Nwanko Kanu alikuwa ni mmoja wa wachezaji walioshinda ubingwa wa EPL msimu wa 2003- 2004 bila kupoteza mchezo wowote pamoja na mastaa wengine kama, Thierry Henry, Jens Lehmann, Patrick Vieira, Freddie Ljungberg na Sol Campbell.
Aliichezea timu ya taifa ya Nigeria kwa mara ya kwanza mwaka 1994 katika mchezo dhidi ya Sweden, amecheza jumla ya mechi 87 akiifungia magoli 12 na amestaafu akiwa amecheza michuano mitatu ya kombe la dunia, michuano ya mwisho ni ya mwaka 2010 iliyofanyika nchini Afrika ya kusini.