Kiongozi wa kanisa katoliki Papa Francis amesema yuko katika upande wa wahanga wa zaidi ya mapadre 300 waliofanya unyama wa unyanyasaji mkubwa kingono nchini Marekani wanaoshutumiwa kuwafanyia unyanyasaji zaidi ya watoto 1000.
Unyama huo ulifanyika katika kipindi cha miongo saba, yameeleza makao makuu ya kanisa Katoliki mjini Vatican.
Wahanga watambue kuwa papa yuko upande wao, imesema taarifa ya Vatican baada ya ripoti mbaya ya jopo la mahakama nchini Marekani kuchapishwa siku ya Jumanne inayoelezea hatua za kuficha madhila hayo zilizofanywa na kanisa Katoliki.
"Kuna maneno mawili yanayoweza kueleza hisia zinazokabili uhalifu huu wa kutisha, aibu na masikitiko. Papa anachukulia kwa dhati kazi ya jopo la mahakama pamoja na ripoti iliyotoa. Papa analaani bila kiasi unyanyasaji kingono watoto wadogo. Unyanyasaji ulioelezwa katika ripoti ni uhalifu na kiroho ni wa kukemewa.
Vitendo hivyo ni usaliti wa imani ambayo imewapora wale waliofanyiwa utu wao na, pia imani yao. Kanisa linapaswa kujifunza somo gumu kutoka yale yaliyopita, na kunahitajika kuwajibika kwa wale waliofanya vitendo hivyo na wale ambao waliruhusu unyanyasaji huo kutokea."
Hayo ni maneno katika taarifa ya makao makuu ya kanisa Katoliki mjini Vatican iliyosomwa na msemaji wa kanisa hilo Greg Burke. "Wale ambao wameathirika ndio anaowapa umuhimu wa kwanza, na kanisa linataka kuwasilikiza ili kuondoa maafa haya ya kutisha ambayo yanaharibu maisha ya watu wasio na hatia," taarifa ya Vatican imesema.