Rais John Magufuli amesema Tanzania na Uganda zitaendelea kufanya biashara kwa pamoja ili kuimarisha uchumi wa nchi zote mbili na kudumisha mshikamano kati yao.
Hayo yameelezwa leo Alhamisi Agosti 9, Ikulu jijini Dar es Salaam wakati Rais Magufuli akizungumza baada ya mazungumzo yake na Rais Yoweri Museven ambaye aliambatana na viongozi mbalimbali kutoka nchini Uganda.
“Nimefurahia sana ziara ya mzee wetu Museven pamoja na ujumbe aliokuja nao hivyo ningependa Tanzania na Uganda tufanye biashara kwa pamoja na tuwe kama ndugu,” amesema Magufuli
Aidha rais Magufuli amesema wamekaa na Rais Museven na kukubaliana kutafuta namna ya kuzuia watu wenye lengo la kuharibu viwanda vya Uganda kutokana na hali hiyo kuwahi kutokea kipindi cha nyuma
“Kuna sukari iliwahi kuingizwa hapa nchini kumbe ilikuwa haijatengenezwa na viwanda vya Uganda bali ilikua na lengo la kuharibu viwanda vyao hivyo tumezungumza na rais Museven ili suala hilo lisijitokeze tena,” amesema Rais Magufuli
Rais Museven yupo nchini kwa ziara ya kikazi yenye lengo la kuimarisha ushirikiano na ujirani mwema uliopo kati ya Tanzania na Uganda.