Akizungumza na vyombo vya habari , Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema Mkapa atakuwa mgeni rasmi katika madhimisho hayo akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.
Amesema pia katika kilele cha Maadhimisho ya maonesho hayo viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali watashiriki wakiwemo Katibu Mkuu wa CCM , Dkt. Bashiru Ally Sambamba na Mawaziri, Manaibu Waziri na Makatibu Wakuu na Manaibu Katibu Mkuu wa wizara mbalimbali.
“Watakuwepo viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali pamoja na viongozi wa Taasisi mbalimbali za Fedha wakiwemo Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania(BOT) Prof. Florens Luoga na Mkurugenzi wa Benki ya NBC, Theobald Sabi”
“Wageni wengine ni Wakurugenzi wa Benki ya NBC na NMB pamoja Viongozi waandamizi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa, hivyo napenda kuwakaribisha wananchi wote wa Mikoa ya Mara, Shinyanga na kwa msisitizo wananchi wa Simiyu ambao ndiyo mkoa mwenyeji kujitokeza kwa wingi kushuhudia maadhimisho ya maonesho haya ambayo ni mara ya kwanza kufanyika Mkoani kwetu” alisema.
Katika hatua nyingine Mtaka amewahakikishia wananchi kuwa usafiri wa kufika katika Uwanja wa Nanenane utakuwa wa uhakika kwa kuwa mabasi ya kwenda huko yapo ya kutosha na nauli zimepunguzwa kutoka Lamadi mpaka Nyakabindi na kutoka Mjini Bariadi kwenda Nyakabindi.