Juzi, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ilifanya mnada makontena hayo katika eneo la bandari kavu ya Malawi Cargo, lakini yalikosa wanunuzi baada ya waliojitokeza kushindwa kufika bei iliyotakiwa.
Jana Makonda alikwenda katika Kanisa la Anglikana wilayani Ngara, Mkoani Kagera ambako iliendeshwa ibada maalumu ya kuzuia mnada wa makotenda yenye samani za walimu wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Makonda ambaye yupo kwenye msiba wa mama mkubwa wa mkewe, alishiriki ibada hiyo na aliwaambiwa waumini wa kanisa hilo kuwa amesali pamoja nao kwa sababu anaamini Mungu ndiye aliyempa makotenda hayo kwa ajili ya walimu wa Mkoa wake.
Alionya kuwa atakayenunua makontena hayo atalaaniwa yeye na uzao wake wote kwa sababu vya madhabahuni havichezewi.
“Nimekwenda katika ibada ya Jumapili katika Kanisa la Anglikana mjini Ngara, nimefanya ibada maalumu kuhakikisha makontena hayo hayapati wateja kwa kuwa naamini Mungu alinipa kwa ajili ya walimu wa mkoa wangu,” anasema Makonda.
RC Makonda anadai kupatikana kwa samani hizo ni jitihada zake binafsi za kuboresha mazingira ya kufanyia kazi walimu ikiwa ni kumuunga mkono Rais John Magufuli aliyeamua kutoa elimu bure kwa Watanzania na hasa watoto wa masikini.
“Rais alitambua umuhimu wa elimu ndiyo maana kama msaidizi wake sikuona sababu ya kukaa kimya wakati mazingira ya walimu si rafiki na kusubiri kuwalaumu pale watoto wanapofeli bila kufanyia kazi changamoto zao.
“Baada ya kuona jitihada za Rais katika sekta ya elimu, kwa kutoa elimu bure nami nikawaza kama msaidizi wake, nafanya nini kuunga mkono kazi nzuri anayoifanya Rais.”
“Ndipo Mungu aliweka wazo lake ndani ya moyo wangu juu ya ujenzi wa ofisi za walimu kama sehemu ya kuboresha mazingira yao. Kwa utukufu wake Mungu, akaandaa watu wa kuchangia tena kutoka nje na ndani ya nchi,” alisema Makonda.
Akitumia maneno ya vitabu vitakatifu, Makonda alisema utukufu wa Mungu umejidhihirisha kwa Watanzania kuchangia, wakiwemo askari wa Jeshi la Kujenga Taifa waliojitolea kujenga majengo; benki kwa kununua saruji; baadhi ya viwanda kutoa mabati na nondo na wengine kujitolea masinki, mabomba na taa.
Makonda alisema nchi ya China imejenga ofisi, huku Watanzania wanaoishi Marekani wakimpatia samani za walimu ambazo zipo kwenye makontena zaidi ya 20 yaliyokwama bandarini yakidaiwa kodi.
“Wananchi na vyombo vya habari wamejitolea na kuendelea kuhamasisha, huku walimu wakichanga kama sehemu ya kujikomboa.
“Cha kushangaza leo vinapigwa mnada ili kutoza kodi kwa kuwa tu makontena yameandikwa Makonda basi kama jina langu hawalipendi watafakari mzigo alionao mwalimu wa Dar es Salaam anayegombea kiti na mwanafunzi anayekaa chini.
“Inasikitisha sana leo TRA inapiga simu kuomba shule binafsi zikanunue vifaa vilivyoletwa kwa msaada na Watanzania kwa ajili ya Watanzania wenzao.
“Ninachoweza kusema tu waliopewa madaraka wawe na hofu ya Mungu, mimi sikalii viti hivyo hata kama msingi wake ni chuki mchukieni Makonda lakini si walimu,” alisema Makonda.
Makonda alisema, “Nakuhakikishia atakayenunua hivi vifaa vya walimu amelaaniwa yeye na uzao wake na kamwe hatafanikiwa katika maisha yake. Nayasema haya nikiwa na uhakika kwa kuwa vya madhabahuni havichezewi.”
“Hivi ni vifaa kwa ajili ya walimu wa mkoa wa Dar es Salaam, Mungu hakunipa kwa ajili ya baa wala kumbi za starehe,” alisema Makonda.