Sababu ya Bocco kukaa benchi mechi za Uturuki
0
August 05, 2018
NA ELBOGAST MYALUKO
Baada ya mshambuliaji wa Simba John Bocco kukosekana katika mechi mbili za kirafiki ilizocheza timu yake nchini Uturuki ilipoweka kambi, idara ya mawasiliano yaweka wazi kuwa nyota huyo anapewa muda wa kupona vizuri.
Bocco ambaye ni nahodha wa Simba, amekosa mechi mbili za kirafiki, ambazo ni dhidi ya Mouloudia Oudja ya Morocco iliyopigwa Agosti 1, 2018 na ile ya F.C.E Ksaifa ya Palestina iliyopigwa jana Agosti 4.
Taarifa kutoka idara ya mawasiliano ya klabu hiyo imeeleza kuwa Bocco ambaye aliumia kwenye mechi za mwisho wa ligi anaendelea na programu maalum ili zimsaidie kupona vizuri na kurejea akiwa kwenye ubora.
Katika mechi hizo mbili Simba ilitoka sare ya bao 1-1 na Mouolodia FC bao la Simba likifungwa na Adam Salamba kabla ya kushinda mabao 3-1 jana dhidi ya F.C.E Ksaifa, mabao ya Emanuel Okwi mawili na Meddie Kagere moja.
Aidha taarifa pia imeeleza kuwa timu hiyo inatarajiwa kuanza safari leo ya kurejea jijini Dar es Salaam tayari kwa mechi ya tamasha la Simba Day itakayopigwa Agosti 8 dhidi Asante Kotoko kwenye uwanja wa taifa jijini Dar es salaam.
Kwa mujibu wa takwimu rasmi, John Bocco ambaye leo anasherehekea siku yake ya kuzaliwa, ndiye mfungaji bora wa muda wote wa ligi kuu soka Tanzania bara akiwa amefunga mabao 97 ndani ya miaka kumi aliyocheza akiwa na klabu za Azam FC na Simba SC.
Tags