Seneta John McCain, shujaa wa vita vya Vietnam aliyehudumu kwa muda mrefu kama seneta nchini Marekani na aliwahi kuwania urais, amefariki dunia akiwa na miaka 81.
Bw McCain, ambaye jina lake kamili ni John Sidney McCain III, alifariki dunia Jumamosi akiwa amezungukwa na jamaa zake, kwa mujibu wa taarifa fupi iliyotolewa na afisi yake.
Alikuwa amegunduliwa kuwa na saratani hatari ya ubongo iliyokuwa inasababisha uvimbe kwenye ubongo wake 2017.
Amekuwa akipokea matibabu tangu wakati huo.
Familia yake hata hivyo ilitangaza kwamba seneta huyo ambaye aliondoka Washington Desemba na kuacha majukumu ya useneta kwenda kupokea matibabu aliamua kuacha kupokea matibabu Ijumaa.
Bintiye McCain, Meghan amesema jukumu kuu alilo nalo maishani sasa litakuwa ni “kuishi kwa mfano wake (McCain), kutimiza matarajio yake na kufikia kiwango chake cha upendo.”
“Siku na miaka ijayo haitakuwa vile tena bila baba yangu – lakini zitakuwa siku njema, zilizojaa uhai na upendo, kwa sababu ya mfano mwema aliokuwa maishani mwake,” ameandika kwenye Twitter.
Seneta huyo aliyehudumu bungeni kwa mihula sita aliwania urais mwaka 2008 kupitia chama cha Republican lakini akashindwa na mgombea wa chama cha Democratic, Barack Obama.
Madaktari waligundua alikuwa anaugua saratani ya ubongo walipokuwa wanamfanyia upasuaji kuondoa damu iliyokuwa imeganda kichwani juu ya jicho lake la kushoto Julai mwaka jana.
McCain alikuwa mwana na mjukuu wa maafisa wakuu katika jeshi la wanamaji nchini Marekani alikuwa rubani wa ndege za kivita wakati wa vita vya Vietnam.
Ndege yake ilitunguliwa vitani na akakaa miaka mitano kama wateka wa wakati wa vita.
Akiwa mateka, aliteswa sana jambo lililomfanya kulemaa, ulemavu ambao aliishi nao maisha yake.