Hatua hiyo imekuja baada ya waandaaji wa mashindano hayo kuanzisha mchakato wa kuunda sheria mpya juu ya mavazi yanayohitajika katika mchezo huo.
Akizungumzia juu ya utaratibu huo mpya utakaoanzishwa, Rais wa shirikisho la tenisi nchini Ufaransa, Bernad Giudicelli amesema "mavazi hayo hayatokubalika tena, ninaamini kuna kitu ambacho sisi tumekwenda mbali sana, unatakiwa kuheshimu mchezo na mahali husika".
Japokuwa Rais huyo hakutaja hasa jinsi gani sheria hiyo itakavyokuwa lakini amesema wana mpango wa kulingana na sheria za mavazi za mashindano ya Wimbledon, ambayo wachezaji wote hulazimika kuvaa mavazi yenye rangi nyeupe pekee.
Kwa upande wake Serena Williams amesema kuwa, mavazi hayo yanamsaidia kuendana na tatizo lake la kuganda kwa damu, tatizo ambalo lilinusurika kumgharimu maisha yake wakati wa kujifungua.
Bingwa huyo mara 23 wa Grand Slam alirejea katika kinyang'anyiro hicho kwenye michuano ya French Open mwezi Mei, kufuatia kumalizika kwa likizo yake baada ya kujifungua mtoto wa kike mwezi Septemba mwaka 2017.
Serena anatarajia kuusaka ubingwa wa saba wa taji la michuano ya US Open itakayoanza Jumatatu ya wiki ijayo, atakapopambana na mwanadada raia wa Poland, Magda Linette anayekamata nafasi ya 60 katika viwango vya tenisi duniani kwa sasa.