Serikali Kumnyang’anya Mohammed Enterprises Mashamba.


Na. Hassan Mabuye, Wizara ya Ardhi
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Angeline Mabula amesema serikali imekusudia kuchukua baadhi ya mashamba yanayomilikiwa na Kampuni ya Mohammed Enterprises na kuwapa wananchi kwa kuwa wameshindwa kutimiza masharti ya endelezaji wake.

Mhe. Mabulla amesema hayo baada ya kufanya ziara ya ukaguzi wa mashamba katika Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga ambapo amegundua kampuni ya Mohammed Enterprises inamiliki maeneo makubwa sana kwa zaidi ya hekta 9,418 sawa na hekari 20,779 ambayo wamechukulia mkopo kwa ajili ya kupanda mkonge, kitu ambacho hakijafanyika kwa asilimia kubwa.

“Hii kampuni ya Mohammed Enterprises imetupa taarifa ambazo si za kweli kwamba wameendeleza maeneo yao wanayoyamiliki kwa asilimia 83, mimi nimefika katika mashamba yote 14 wanayoyamiliki na nimeona ni eneo kubwa sana ambalo limebaki pori na halijapandwa mkonge tangu wakabidhiwe mwaka 2000 takribani miaka 17 sasa wakati wananchi wa Korogwe wanakosa maeneo ya kulima, kuishi na kufugia” amesema Mhe. Mabula.

“Kwa sasa Wizara yangu imejiridhisha kwamba kuna haja ya kugawa maeneo yanayomilikiwa na Mohammed Enterprises ambayo hayajendelezwa kwa kupandwa mkonge ili wapewe wananchi wa Korogwe ambao wana uhaba wa ardhi kwa muda mrefu kutokana na maeneo makubwa kumilikiwa na watu wachache”. Mhe. Mabula ameongeza.

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Angeline Mabulla amefanya ziara ya ukaguzi wa mashamba yote 14 yanayomilikiwa na Kampuni ya Mohammed Enterprises na kugundua kuwa amepanda mkonge eneo dogo sana na sehemu kubwa ni mapori tofauti na taarifa aliyopewa na kampuni hiyo.

Waziri pia amesema mashamba hayo yametumika kuchukua mikopo benki lakini mikopo hiyo haijatumika kuendeleza mashamba hayo kitu ambacho kinafanya wananchi wayahitaji maeneo hayo lakini wanashindwa kuyatumia kwa kuwa yanamilikiwa na kampuni ya Mohammed Enterprises.

Akijatetea mbele ya Naibu Waziri wa Ardhi Meneja anayesimamia Mashamba yote ya mkonge ya kampuni ya Mohammed Enterprises ndugu Newalo Nyari mesema kwamba si kweli kwamba hawajaendeleza maeneo hayo bali wameendeleza na wamepanda mkonge baadhi ya maeneo na mengine wameyaacha mapori ili kuhifadhi misitu na mengine wanawaachia wananchi waweze kupanda mazao yao ikiwa ni ushirikiano wa kijirani.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Handeni aliyekuwa akikaimu nafasi ya Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Mhe. Godwine Gondwe ambaye ameonesha kukasirishwa na maneno ya meneja huyo kwamba wameendeleza mashamba hayo wakati yeye mwenyewe ameshuhudia kwa macho yake mashamba yote 14 na kuona hali halisi ya mapori ambayo hayaendelezwa.

Baadhi ya wananchi wa Korogwe wameonesha kufurahishwa na hatua hiyo ya Serikali ya kuipunguzia umiliki wa baadhi ya maeneo yanayomilikiwa na kampuni ya Mohammed Enterprises ambayo watapewa wananchi hao ili waweze kufanya shughuli zao za maendeleo.

Hata hivyo kwa mujibu wa sheria ya ubatilishaji umiliki wa mashamba ni Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ndiye mwenye dhamana ya kumyanga’anya mmiliki wa ardhi au mashamba baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Waziri wa Ardhi.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad