Katika hatua ya kukabiliana na uhaba wa saruji nchini, serikali imezuia usafirishaji wa bidhaa hiyo na makaa ya mawe kwenda nje ya nchi kabla ya kutosheleza kwanza soko la ndani ya nchi.
Hatua hiyo imefikiwa ili kuwezesha saruji inayozalishwa nchini kuwanufaisha kwanza watanzania na kuwezesha utekelezaji wa miradi mikubwa ya ujenzi inayoendelea hivi sasa.
Pia serikali imeahidi kuboresha miundombinu ya kwenda na kutoka kwenye viwanda vya kuzalishia saruji na makaa ya mawe ili bidhaa hizo zisafirishwe kwa haraka na ufanisi kwenda sokoni.
Hatua hiyo inakuja wakati takribani wiki mbili sasa kumekuwa na uhaba wa saruji nchini hatua iliyosababisha ongezeko la juu la bei ya bidhaa hiyo huku maeneo mengine ikikosekana kabisa.
Ili kuweza kupata ufumbuzi wa kudumu wa sakata hilo, juzi Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Stella Manyanya alifanya mkutano na wazalishaji, wasambazaji, wasafirishaji wa saruji na kampuni zinazozalisha makaa ya mawe.
Kikao hicho kilichodumu kwa takribani saa tatu kilianza saa moja jioni na kumalizika saa nne usiku, huku Naibu Waziri Manyanya akianza kwa kuwataka wadau hao kulipatia uzito unaostahili jambo hilo kwa kuwa linagusa maslahi ya kitaifa huku akiwasihi kutofanya nalo mzaha.
Aliwatahadharisha kuwa jambo hilo linaweza kuwa na uamuzi mzito au wa kawaida na baadaye alianza kusikiliza maoni ya wazalishaji wa saruji kabla ya kuja kwa wadau wengine.
Baada ya kikao hicho kumalizika, Waziri Manyanya alisoma makubaliano waliyofikia ambapo alisema kwa kuwa kwenye mazungumzo hayo imebainika kuwa kuna kiwango cha saruji ambacho pia huuzwa nje ya nchi, hivyo wamekubaliana kwanza saruji itosheleze soko la ndani kabla ya kuanza kuuzwa nje, vivyo hivyo kwa makaa ya mawe.
Alisema: ”Ili kuhakikisha soko la ndani linajitosheleza kwanza wanatakiwa kuuza kiwango kikubwa ndani ya nchi na kinachobakia ndio iwe nje na hii haimaanishi kuwa hatutaki wauze nje, hapana ila tunachotaka ni kwanza soko la ndani watanzania na miradi mingine ya ujenzi inufaike”.
Aliongeza: ”Ubovu wa miundombinu ya barabara kwenda na kutoka kwenye viwanda vya kuzalishia makaa ya mawe kumesababisha magari kuchukua muda mrefu zaidi kubeba bidhaa hizo na hivyo kuleta uhaba kwa wazalishaji na hivyo wamekubaliana na Wakala Barabara Tanzania”.
Alisema, wiki moja kuanzia sasa kutakuwa na kiwango kikubwa cha saruji mitaani na kuwa kila mdau amekubali kutekeleza walichokubaliana huku akiwataka kutambua kuwa saruji ina mchango mkubwa kwa sasa katika kuelekea kwenye Tanzania ya viwanda hasa kutokana na miradi mikubwa inayoendelea kutekelezwa yenye kuhitaji zaidi bidhaa hiyo.
Credit: Habari Leo