Rapa mkongwe Fid Q, amesema chanzo kikubwa cha baadhi ya wasanii kuonekana wanafanya vibaya katika kazi zao, ni mashindano yanayoibuka baina ya watu wawili na kusababisha athari kwa wengine.
Fid Q amebainisha hayo alipokuwa anazungumza kwenye kipindi cha PLANET BONGO 'PB' kinachorushwa na East Africa Radio, baada ya kuzuka tabia ya baadhi ya mashabiki pamoja na wasanii wenyewe kutengeneza bifu baina ya wasanii wawili kusudi wawe wanaongelewa na kufuatiliwa zaidi.
"Masuala ya mashindano mimi mara nyingi huwa siyakubali sana kwasababu yanatengeneza makundi na timu ambazo zinadumaza watu kushindwa kufikiria vitu vingine pamoja na kazi za watu tofauti wanazokuwa wakifanya na badala yake wasanii wengine wanashindwa kupewa nafasi ya kutosha kwa mashabiki", amesema Fid Q.
Pamoja na hayo, Fid Q ameendelea kwa kusema "kwa hiyo watu wa aina hiyo wanakuwa wanalala katika 'pure arts' nyingine. Wasanii wengi wanakuja lakini watu wanakuwa hawana muda na wao na kuhitaji ushindani uliokuwepo wa pande mbili yaani Simba na Yanga".
Mbali na hilo, Fid Q amesema kwa upande wake hana mtu wa kushinda naye kutokana na kazi anazozifanya kutofanana na mwingine.
"Mimi binafsi sina 'challenge' kwa maana nimekuwa nikifanya kazi zangu kwa muda mrefu na simuoni mtu ambaye ananipa upinzani", amesisitiza Fid Q.
Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na tabia ya baadhi ya mashabiki kuwashindanisha wasanii wawili tofauti kwa mlengo wa kutaka kujaribu kuchangamsha 'game', licha ya kuwa kwa upande mmoja jambo hilo hutoa athari kwa wasanii wengine ambao hawapo katika kundi hilo.