Zikiwa zimepita siku mbili baada Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutangaza kuwatema wachezaji sita wa Simba waliokuwa wameitwa katika kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars, mmoja wa wachezaji hao amefunguka kuhusiana na suala hilo.
TFF iliwatema katika kikosi hicho John Bocco, Shiza Kichuya, Jonas Mkude, Erasto Nyoni, Shomari Kapombe pamoja na Hassan Dilunga kwa kosa la kuchelewa kujiunga na kambi ya Taifa Stars kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wa kimataifa wa kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) dhidi ya Uganda.
Akizungumza na Championi Ijumaa kwa sharti la kutotajwa jina lake, mchezaji huyo alisema TFF imewaonea kutokana na hatua hiyo, pia imesababisha jamii iwaone kuwa ni watu wasiokuwa na moyo wa uzalendo kwa nchi yao.
Alisema taarifa walizopewa kuhusiana na kujiunga na kambi hiyo ya Taifa Stars, walizielewa kwamba walitakiwa wajiunge na timu hiyo juzi Jumatano saa 6:00 mchana na siyo Jumanne saa 12 jioni.
“Meseji ya kwanza kabisa ya kututaka tujiunge na kambi ya timu ya taifa tulipata Jumanne saa moja jioni kutoka kwa meneja wetu, Richard Robert na ilianza kwa kusema kuwa ‘mechi ya tarehe mbili dhidi ya Lipuli imesitishwa, kwa hiyo wachezaji wote mliopo timu ya taifa mripoti Sea Scape kesho (juzi Jumatano) saa sita mchana.
“Meseji hiyo imeandikwa kwa Kiswahili lakini pia kwa Kingereza, kwa hiyo kutokana na hali hiyo na sisi jana (juzi) Jumatano kabla ya saa sita mchana wote tulikuwa tumeishafika kambini.
“Lakini baada ya kufika tuliambiwa kuwa hatutakiwi kwa sababu tumechelewa na tulipojaribu kujitetea tuligonga mwamba, hivyo ikatubidi tuondoke zetu, kwa hiyo ukweli ndiyo huo ila kama kweli tulitakiwa kufika Jumanne saa kumi na mbili jioni basi tulipotoswa na waliotupatia taarifa,” alisema mchezaji huyo.
Alipotafutwa Robert hakupatikana kutokana na simu yake ya mkononi kuita tu bila kupokelewa.
Hata hivyo, kesho Jumamosi Robert pamoja na Kaimu Katibu Mkuu Simba, Hamis Kisiwa wanatarajiwa kuhojiwa na Kamati ya Maadili ya TFF kutokana na kosa la kushindwa kutimiza wajibu wao wa kuhakikisha wachezaji wao wanaripoti kambini mapema kama walivyoagizwa na shirikisho hilo.
Wachezaji walioitwa kuchukua nafasi za wachezaji wa Simba walioondolewa katika kikosi hicho ni Paul Ngalema wa Lipuli, Salum Kimenya (Prisons), David Mwantika na Frank Domayo (Azam), Salum Kihimbwa na Kelvin Sabato (Mtibwa Sugar).