Rapa mkongwe nchini Tanzania, Dudu Baya amefunguka na kudai haitakuja kutokea maishani mwake kutoa fedha na kumpatia mwanamke ili kusudi aende kutoa mimba kwani yupo tayari kula ugali kwa dagaa lakini sio kushiriki kwenye dhambi ya aina hiyo.
Dudu Baya ametoa kauli hiyo wakati alipokuwa anazungumza kwenye kipindi cha FRIDAY NIGHT LIVE 'FNL' kinachorushwa mubashara na EATV kila siku ya Ijumaa kuanzia saa 3:00 za usiku, baada ya kuwepo tabia ya baadhi ya wanaume na wanawake kushirikiana kwa pamoja katika kitendo cha kutoa mimba kwa kigezo cha kuwa bado hawajajipanga vizuri kimaisha.
"Mimi ni mwanaume ambaye siwezi kushiriki kwenye tendo la kumpa mwanamke pesa aende akatoe mimba. Ila kuna wanaume wenye hela nyingi au vyeo vikubwa wanaweza wakampa mwanamke hata millioni 10 aende akatoe mimba, kusudi walinde heshima na vyeo vyao lakini mimi hiyo dhambi siwezi kuifanya", amesema Dudu Baya.
Pamoja na hayo, Dudu Baya ameendelea kwa kusema "endapo ikatokea nimempa mimba mwanamke basi asijidanganye kama nitampa hata shilingi 10 aende akaitoe, nitalea hiyo mimba pamoja na mtoto akizaliwa hata kama tutakula ugali kwa dagaa kwasababu hayo ni maisha tu".
Mbali na hilo, Dudu Baya amekanusha 'skendo' zilizokuwa zikisambazwa kwenye mitandao ya kijamii katika siku za hivi karibuni kuwa ametelekeza mtoto wake anayeitwa William Godfrey maarufu kama Wille Dudu, na kudai sio za kweli kwani mtoto huyo alimlea yeye mwenyewe na kumsomesha shule mbalimbali.
"Mtoto wangu nimeishi naye mwenyewe kwa miaka 14, lakini alipokuja kutana na mama yake ndipo alianza kubadilika, akanza kufanya muziki kimya kimya bila ya mimi kujua, mbaya zaidi akaambiwa asije kushirikiana nami kwa kuwa nyimbo zangu zinafungikiwa kwasababu hazina maadili, na kumtaka washirikiane wao wenyewe wawili kwa imani watakuja kupata mafanikio makubwa kama alivyopata msanii fulani hapa bongo aliyedai kutengwa na baba yake katika ukuaji wake", amesisitiza Dudu Baya.
Wille Dudu alizua gumzo kubwa mitandaoni kwa kile alichokuwa akidai anaishi kwenye mazingira magumu licha ya baba yake kuwepo.