CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimewataka wanachama wa chama hicho kuondoa hofu kufuatia wabunge na wanachama wanaokihama kwenda Chama cha Mapinduzi (CCM) na kueleza huo ni mtikisiko wa kawaida ambao hautaathiri mabadiliko.
Akihutubia mkutano wa kampeni za udiwani Kata ya Makorola, mkoani Tanga, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Zanzibar, Salum Mwalimu,
alisema wanaojisalimisha CCM hawawezi kuathiri nguvu ya mabadiliko iliyopo kwa kuwa hao si wanaharakati wa kweli, ni sawa na kenge kwenye msafara wa mamba.
Mwalimu alisema kuikosoa, kushauri na kufichua mambo mabaya ya serikali ndiyo wajibu wa vyama vya upinzani hivyo wataendelea na kazi hiyo ili kujenga uwajibikaji na uadilifu na kamwe hawatafunga midomo.
“Hawa jamaa wana mtindo ukisema kidogo unaitwa polisi kutoa maelezo sasa mimi natembea kabisa na maelezo yangu kwenye karatasi nikiitwa tu badala ya kupoteza muda kuyaandika nakabidhi tu,” alisema Mwalimu.
Aliwataka wananchi kutosikiliza propaganda za kisiasa kuhusu uchumi na maendeleo yao kwa ujumla kwa kuwa kila Mtanzania anaona hali ya maisha ilivyo baada ya serikali kushindwa kuendeleza, kufufua na kujenga viwanda licha ya kaulimbiu yake ya Tanzania ya viwanda.
Aliwaomba wakazi wa kata hiyo kumchagua mgombea kwa tiketi ya Chadema, Zainab Ashiraf, ambaye anaungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Naye Diwani wa Kata ya Tabata, Jimbo la Segerea jijini Dar es Salaam, Patrick Asenga, alisema kushuka kwa mapato kwenye halmashauri kunatokana na serikali kupora vyanzo vyote vya mapato na kuziacha kama yatima zikiwa hazina pesa.
Awali, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi CUF, Wilaya ya Tanga, Amour Abal-Hasan, alisema ushiriki wa chama chake kwenye kampeni hizo unatokana na umoja wao wa Ukawa na kwamba CUF iliyomsimamisha mgombea wake ni ya wasaliti.
Mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Tanga, Rashid Jumbe aliwataka wanachama wa vyama vya upinzani na wa CCM pia wamchague mgombea wa Ukawa mwenye uwezo na nia thabiti ya kuleta mabadiliko kwenye kata hiyo.