TCU: Kesho Ndo Mwisho wa Kutuma Maombi ya Kujiunga Chuo Kikuu Shahada ya Kwanza

TCU: Kesho Ndo Mwisho wa Kutuma Maombi ya Kujiunga Chuo Kikuu Shahada ya Kwanza
Tume ya vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imesema kuwa kesho Agosti 15, 2018 ndiyo mwisho wa kutuma maombi ya kujiunga na masomo ya shahada ya kwanza katika vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu nchini.

Dirisha hilo la kuwasilisha maombi lilifunguliwa Julai 20, 2018 kwa awamu ya kwanza.

Akizungumza leo Agosti 14, 2018 Katibu Mtendaji wa TCU Profesa Charles Kihampa amesema kuwa baada ya kufungwa rasmi kwa dirisha la udahili vyuo vitaanza kuchakata majina ya waombaji kulingana na vigezo vya udahili vilivyowekwa kwa kila programu ya masomo.

Udahili wa kujiunga na vyuo vikuu unahusu makundi makubwa matatu ambayo ni waombaji wa kidato cha sita, wenye sifa linganifu kama vile shahada  na waombaji wenye vyeti toka nje ya nchi vyenye sifa linganifu.

"Baada ya kuchakata majina, dirisha la waombaji litaidhinishwa, " amesema Kihampa na kuongeza:

"TCU jukumu lao ni kuhakiki kama waombaji waliochaguliwa na vyuo wana sifa stahiki na wanakidhi vigezo vya kujiunga na programu husika za masomo,"amesema Profesa Kihampa.

Amefafanua kuwa waombaji wote wa udahili wanapaswa kutuma maombi yao moja kwa moja kwenye vyuo wanavyopenda na kuchagua programu za masomo.

Amesema Tume imetoa mwongozo wa programu zilizoidhinishwa kudahili pamoja na vigezo vya udahili vinavyotakiwa kwa kila programu za masomo.

"Waombaji wote wa vyuo vikuu na taasisi ya elimu ya juu wanakumbushwa na kuhimizwa kuzingatia kalenda ya udahili iliyoidhinishwa na Tume,"amesema Kihampa  na kuongeza:

"Ili kuepusha usumbufu usio wa lazima, waombaji wote wanahimizwa kutumia muda uliobaki kukamilisha maombi yao.”

Kihampa amesema dirisha la kuwasilisha maombi ya kujiunga na vyuo vya elimu ya juu awamu ya pili litafunguliwa Septemba tatu hadi saba.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad