UONGOZI wa Coastal Union ‘Wagosi wa Kaya’ umesema kuwa malengo yao msimu huu katika Ligi Kuu Bara ni kushinda kila mechi watakayoteremka uwanjani iwe nyumbani au ugenini na hakuna wa kuwazuia kwani wana wachezaji wenye uwezo wa kufanya hivyo.
Coastal ambao hivi karibuni wamemsajili mwanamuziki Alikiba, kwa sasa wanaendelea na mazoezi kwenye Uwanja wa Saruji yanayosimamiwa na makocha, Juma Mgunda, Joseph Lazaro pamoja Salim Waziri (Tupa).
Makamo Mwenyeketi wa Kamati ya Usajili, Abdallah Mohamed (Wiya) amesema usajili waliofanya kwa wachezaji wazoefu na chipukizi ndiyo sababu kubwa ya kuamini watafanya vizuri msimu huu.
“Malengo yetu kwanza ni kuhakikisha tunashinda michezo hii mitatu ya nyumbani dhidi ya Lipuli FC, Biashara United na KMC baada ya kuzipata hizo ndiyo itatuongezea hamasa ya kwenda kufanya vizuri katika mechi za ugenini zinazofuata,” alisema Wiya.
Kocha wa timu hiyo, Juma Mgunda alisema wachezaji wote wapo fiti na wanaendelea na mazoezi vizuri, wapo tayari kwa mapambano yoyote ila la muhimu ni wadau wa michezo mkoani hapa kuendelea kutuunga mkono.
Adam Mwanyakunga, Tanga
Timu ya Coastal Union Yaanza Mikwala Kabla Ligi Haijaanza Baada ya Kumsajili Kiba
0
August 13, 2018
Tags