Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imetoa ufafanuzi juu ya maswali yenye utata kuhusiana na sakata la makontena 20 yaliyo Bandari ya Dar es Salaam ambayo sasa yapo mnadani.
Makontena hayo ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda yalikuwa yanadiwe Jumamosi iliyopita, lakini yalikosa wanunuzi baada ya watu wengi kushindwa kufikia bei iliyotangazwa.
Kushindwa kuuzika kwa makontena hayo kulimuibua Makonda aliyetishia kuwa atakayeyanunua atamlaani pamoja na uzao wake wote vitisho ambavyo havikumfurahisha Waziri wa Fedha na Mipango, Philip Mpango ambaye Jumatatu alifanya ziara bandarini kuyakagua makontena hayo huku akiagiza yauzwe na kuwataka watu wasiogope vitisho vyovyote.
Pamoja na maelezo ya Waziri na TRA, bado kulikuwa na utata juu ya sakata hilo huku kukiibuka maswali kutoka maeneo mbalimbali na kwenye mitandao ya kijamii.
Akizungumza na Mwananchi jana, mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo alifafanua kuhusu maswali na utata huo huku akisisitiza kuwa vifaa hivyo vitauzika tu. Miongoni mwa maswali hayo ni je, makontena hayo yamebeba samani tu au kuna vitu vingine ndani?
Akijibu swali hilo, Kayombo alisema mamlaka hiyo imethibitisha kuwa makontena hayo yamekuja bandarini yakiwa na samani pekee ikiwamo viti, meza na mbao za kuandikia na si vinginevyo. “Sisi tumeona samani tu,” alijibu kwa ufupi.
Je, ni makontena 36 au 20
Suala la pili ni juu ya kutofautiana kwa taarifa za uagizaji wa makontena hayo ambapo taarifa za awali kwa mujibu wa mtandao wa gazeti la Serikali la Habari Leo zinasema Mkuu wa Mkoa alipokea makontena 20 ikiwa ni sehemu ya shehena ya makontana 36.
Jana, kupitia akaunti yake ya Twitter, mwanahabari na mkurugenzi wa kampuni ya Compass Communications, Maria Sarungi aliandika;
“Februari 16 habari ilitolewa kuwa RC (Mkuu wa Mkoa) amepokea makontena 20 kati ya 36 yenye samani, sasa TRA makontena 16 yako wapi?” aliuliza.
Akijibu Kayombo alisema awali, mamlaka hiyo ilipokea barua ambayo iliyaombea msamaha makontena 36 kabla ya muagizaji kufanya mabadiliko na kuomba makontena 20 yasamehewe kodi.
“Ni kwamba barua ya maombi ya kwanza waliombea msamaha makontena 36, hatahivyo, baadaye kulikuwa na mabadiliko ya maombi kwa ajili ya makontena 20 na yameshafika,” alisema.
Nani anastahili msamaha wa kodi?
Baada ya TRA kukataa kutoa msamaha wa kodi kwa mali hizo kama ilivyoombwa na muagizaji (Paul Makonda) kumekuwa na maswali ya nani anastahili msamaha huo?
Akielezea jambo hilo, Kayombo alisema mali zote zinazotoka nje ya nchi ambazo zipo katika kundi la samani zinatakiwa kulipiwa kodi bila kujali aina ya taasisi au wadhifa wa muagizaji.
“Samani zozote kutoka nje ya nchi zinalipiwa kodi, hata awe ameagiza nani ni lazima zilipiwe kodi kwa ajili ya kuwa-encourage (kuhamasisha) watu kununua samani zinazotengenezwa ndani ya nchi,”alisema.
Mnada utafanyika lini?
Kayombo alisema TRA itanadi tena vifaa hivyo Jumamosi wiki hii na utajumuisha samani na makontena 20 yaliyopo bandarini. Hatua hiyo inakuja baada ya mnada wa kwanza uliofanyika Jumamosi iliyopita kukosa wanunuzi kutokana na watu waliojitokeza mnadani hapo kushindwa kufikia bei iliyowekwa na TRA ambayo inadaiwa ni Sh60 milioni kwa kila kontena.
Mnada utafanyika mara ngapi?
Pia, kumekuwa na maswali mengi juu ya hatua gani zitachukuliwa endapo makontena hayo yatakosa mnunuzi.
Kayombo alisema mamlaka hiyo inaamini haitakosa wanunuzi kwa sababu kuna watu wengi wanaendelea kuulizia wakiwa na nia ya kununua vifaa hivyo.
“Hatuwezi kukosa wanunuzi, wanunuzi wapo na wengi sana wanaulizia kwa hiyo tunaamini watapatikana. Tunaweza kuuza mara nyingi iwezekanavyo na maamuzi mengine tutafanya mbele kwa mbele.”
Alipotafutwa mkurugenzi wa kampuni ya udalali ya Yono, Scholastika Kavela hakutaka kuzungumza chochote kwa madai yeye ni wakala tu.
Awali, Jumapili iliyopita, Makonda alipoulizwa juu ya hatua atakazozichukua kuhakikisha makontena hayo hayauzwi na badala yake yanapelekwa kwa walimu kama ilivyokusudiwa alisema;
“Leo (Jumapili) nimekwenda katika ibada Kanisa la Anglican mjini Ngara, nimefanya ibada maalumu kuhakikisha makontena hayo hayapati wateja kwa kuwa naamini Mungu alinipa kwa ajili ya walimu wa mkoa wangu,” alisema.
“Rais alitambua umuhimu wa elimu ndiyo maana kama msaidizi wake sikuona sababu ya kukaa kimya wakati mazingira ya walimu si rafiki na kusubiri kuwalaumu pale watoto wanapofeli bila kufanyia kazi changamoto zao,” alisema Makonda.