MBUNGE wa Jimbo la Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu ambaye yupo nchini Ubelgiji akipatiwa matibabu kutokana na majeraha ya kupigwa risasi na watu wasiojulikana mwaka jana akiwa nyumbani kwake Jijini Dodoma muda mfupi baada ya kutoka Bungeni amesema ana mpango wa kurejea Tanzania na kuendelea na majukumu yake kama mbunge punde atakapopewa ruhusa na daktari.
Katika mahojiano na BBC amezungumzia hali inayowakabiliwa wanasiasa wa upinzani nchini na kusema upinzani unakabiliwa na wakati mgumu wa kuendesha siasa na kuikosoa serikali.
“Wapinzani hatujakaa kimya, … viongozi wa upinzani kuanzia Mwenyekiti, Makatibu Wakuu, na baadhi ya wabunge wana kesi mahakamani, wanapigania maisha yao, tuna familia. Unaambiwa uwe mahakamani kila siku ili ujitetee, huo muda wa kwenda kufanya kazi nyingine unakuwa haupo. Lakini kusema kweli hatujanyamaza, ukatili ambao tunakabiliana nao ni mkubwa sana,” amesema.
Lissu anasema pia bunge la Tanzania halijamlipia gharama za matibabu yake tangu alazwe hospitalini. Hata hivyo serikali kwa upande wake ilishaeeleza kuwa Lissu hakufuata utaratibu unaotakiwa wa kupelekwa kwanza katika hospitali ya taifa ya Muhimbili ili aweze kuandikiwa mapendekezo ya kupelekwa na kutibiwa nje ya nchi au katika hospitali nyingine.
Spika wa Bunge la Tanzania Job Ndugai alisema kwamba iwapo utaratibu huo utafuatwa hata sasa, malipo ya huduma zote za matibabu zitalipwa na bunge la Tanzania.