TWAWEZA wafunguka kuhusu barua ya COSTECH na tukio la kuchukuliwa kwa Passport ya Mkurugenzi wao na maafisa uhamiaji


Leo Agosti 03, 2018 Shirika la Twaweza nchini Tanzania limeongea na Waandishi wa Habari kuhusu barua ya kuhoji uhalali wao wa kufanya tafiti nchini waliyopewa na COSTECH, pia kushikiliwa kwa passport ya kusafiria ya Mkurugenzi wao Mtendaji na mafanikio waliyoyapata ndani ya miaka 10 ya kufanya kazi Tanzania.



Soma taarifa zaidi kutoka kwa Twaweza hapa chini walioitoa kwa vyombo vya habari:

Kwa wiki kadhaa zilizopita, Twaweza imetajwa sana na kujadiliwa katika vyombo vya habari na katika mijadala mbali mbali ya umma. Kwa kipindi chote hicho tumekuwa kimya ili kujipatia muda wa kutafakari masuala yote haya kwa kina. Lengo kuu la mkutano wa leo ni kuujulisha umma Twaweza ni nini, tunafanya nini na tunasimamia misingi gani katika utekelezaji wa majukumu yetu. Kupitia mkutano huu tunaamini kwamba tutajibu tashwishwi na maswali mengi ya umma yanayoonekana kuelea bila majibu sahihi.

Awali ya yote tungependa kuwafahamisha matukio ya hivi karibuni yaliyopelekea Twaweza kutajwa na kujadiliwa katika vyombo vya habari na mijadala mingineyo ya umma.

MATUKIO
Kwa wiki kadhaa sasa, Twaweza imepitia kipindi chenye changamoto za mashirikiano baina yake na baadhi ya taasisi za kiserikali kufuatia uzinduzi wa taarifa za ripoti mbili za Sauti za Wananchi mnamo Julai 5, zenye vichwa vya habari; Kuwapasha Viongozi? Na Nahodha wa Meli yetu wenyewe?

Tumepokea barua mbili kutoka Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) ambazo zinahoji uhalali wa programu ya Sauti za Wananchi na kututaka tufafanue kwa nini hatua za kisheria zisichukuliwe dhidi yetu. Tumezijibu barua zote mbili kwa wakati tuliopewa.

Pia Idara ya Uhamiaji imeishikilia pasi Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza ya kusafiria tangu Julai 24. Siku ya Agosti 1, Ndugu Aidan Eyakuze alizuiliwa kusafiri kwa kutumia Shahada ya Dharura iliyotolewa kwa utaratibu uliopo, ili aweze kushiriki mikutano ya kikazi kwenye ofisi za Twaweza jijini Nairobi na Kampala. Hatuna taarifa yoyote ya amri ya kimahakama yenye kuidhinisha jambo hili.

TWAWEZA
Twaweza ni shirika lenye kuamini katika uwazi na linashirikiana kwa ukaribu na wadau muhimu katika jitihada zake za kuchangia katika ukuaji wa demokrasia na maendeleo nchini Tanzania. Mara kwa mara tumefanya kazi na Serikali tumechangia katika jitihada za serikali kwa kufanya tafiti zinazoleta takwimu muhimu katika kuibua mawazo na habari zenye kutoa mwangaza na uhalisia wa mambo katika kujaribu kutafuta ufumbuzi wa maswala mbali mbali muhimu.

Shirika la Twaweza lilianzishwa mwaka 2009 na Mwanaharakati Mtanzania, bwana Rakesh Rajani ikifanya kazi zake nchini Kenya, Tanzania na Uganda kwa lengo la kuhamasisha uwepo wa raia makini (watu kufanya kazi ya kutatua matatizo yao wenyewe, na kushirikiana na serikali inapobidi); mamlaka zenye kuwajibika (serikali sikivu na yenye kuchukua kwa umakini hoja na mawazo ya wananchi); na watoto kujifunza ili waweze kukua na kuwa raia wenye tija na ushiriki.

UWEZO
Moja ya programu kubwa za Twaweza ni Uwezo, tathmini kubwa barani Afrika inayotekelezwa na wananchi wenyewe chini ya uratibu wa Twaweza. Maelfu ya wananchi wamejengewa uwezo wa kukusanya takwimu na kutathmini endapo watoto kati ya umri wa miaka 6 hadi 16 wanaweza kusoma hadithi za kiwango cha darasa la pili kwa lugha ya Kiingereza na Kiswahili na pia endapo wanaweza kufanya hesabu za darasa la pili. Kwa kupitia uhakiki wa karibu na mara kwa mara wa ubora wa elimu na kusambazwa kwa matokeo ya tathmini hii, Uwezo imekuwa ikichangia ukusanywaji wa mamilioni ya dola kuelekezwa katika mfumo wa elimu nchini Tanzania kwa lengo la kuwa na matokeo bora ya kujifunza. Nchi nyingi zinaona thamani na tunu kubwa ya mfumo huu unaotekelezwa na wananchi katika kutathmini matokeo ya elimu kwa watoto, na Uwezo imeshirikiana na serikali na asasi za kiraia katika nchi zaidi ya saba kutoa ushauri wa namna gani watatekeleza vyema jitihada kama hizi.

Pia Twaweza, kupitia programu ya Uwezo, imekuwa ikishirikiana na serikali katika kuhakikisha upatikanaji wa elimu bora kwa watoto wote Tanzania.
Matokeo ya tathmini za Uwezo yaliigutusha serikali kuhusu tatizo la matokeo duni ya elimu, yaani pamoja na kuongezeka idadi ya shule na watoto wanaopelekwa shuleni, bado kuna tatizo kubwa la watoto kujifunza maarifa na kupata stadi muhimu kama kusoma na kufanya hesabu. Hatimaye, sera na mikakati mbalimbali ya serikali imenukuu matokeo haya ya tathmini ya Uwezo, na wabunge na viongozi kadhaa wa serikali wametumia taarifa za Uwezo kwenye mijadala ya kisera kuhusu elimu.
Matokeo ya tathmini za Uwezo yamechochea mijadala ya elimu na maarifa ya kimkakati kwenye takribani wilaya 150 na tumesisitiza umuhimu wa wadau hasa hasa wananchi na serikali za mitaa kushirikiana katika kuboresha sekta ya elimu kwenye maeneo yao.
Kutokana na mchango wa programu ya Uwezo na tafiti nyingine za Twaweza, tumekuwa mwanachama wa kikundi kazi (Task Force) cha kutengeneza Mwongozo wa Taifa wa Tathmini ya Darasa la Pili (National Standard 2 assessment framework)

KiuFunza
Mbali na programu ya Uwezo, kupitia program ya KiuFunza, mradi mkubwa mwingine, iliyofanyika katika wilaya 11 nchini tangu mwaka 2014 mpaka mwaka 2016, Twaweza imeonesha umuhimu na uwezekano wa kupeleka fedha za ruzuku moja kwa moja shuleni bila kupitia Halmashauri za Wilaya.

Jambo hili liliishawishi serikali kutekeleza sera hii ya kupeleka ruzuku moja kwa moja shuleni. KiuFunza pia ililenga kuwalipa walimu bakshishi kutokana na ufanisi wao ili kuwapa motisha kufanya kazi kwa bidii na kuwezesha watoto kujua kusoma na kufanya hesabu kulingana na matarajio ya mitaala ya darasa la 1-3.

Matokeo ya KiuFunza yameipendeza Serikali na sasa tumeingia ubia na TAMISEMI na Wizara ya Elimu kutekeleza mkakati wa kuwapa motisha walimu ili waweze kujituma zaidi kufundisha watoto kwa matokeo bora zaidi.

Sauti za Wananchi
Sauti za Wananchi ni programu nyingine kubwa ya Twaweza. Sauti za Wananchi inatoa fursa kwa wadau wa serikali, wafanya maamuzi, vyombo vya habari na wadau wengine kufahamu hali halisi (ama kupima mapigo ya moyo) kwenye masuala mbalimbali ya kijamii, kisiasa na kiuchumi nchini. Kabla ya programu hii ya Sauti za Wananchi, hapajawahi kuwapo fursa na uwezo kufahamu maoni ya wananchi wa kawaida kwa uharaka na kwa gharama nafuu.

Sauti za Wananchi imekuwa chipukizi na kinara katika nyanja hii ya kupima mapigo ya moyo wa taifa. Ufanisi huu wa kuandaa, kutekeleza na kusimamia programu uliishawishi Benki ya Dunia kushirikiana na Twaweza katika kuandika kwa pamoja kitabu juu ya namna gani tafiti zenye kutumia simu zinaweza kufanywa. Jambo ambalo limebuniwa na kutendwa Tanzania sasa linatumika kama mfano bora na jambo la kuelimisha taasisi katika kila pembe ya dunia.

Idara kadhaa za serikali zimeshatumia taarifa zinazotolewa na Sauti za Wananchi kukusanya takwimu ambazo zinasaidia katika utekelezaji wa kazi zao, ikiwemo Jeshi la Polisi, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Ofisi ya Taifa ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Pia, tumepokea na kushughulikia maombi ya kutoa ripoti za kina kwa baadhi ya maafisa wa serikali.

Sauti za Wananchi ilianzishwa mnamo mwaka 2013 nchini Tanzania na Twaweza iliendesha raundi 65 kwa kutumia miundo mbinu iliyoiweka na kuchapa zaidi ya machapisho 50 toka katika maoni, sauti na uzoefu wa wananchi. Katika kipindi hicho, matokeo ya Sauti za Wananchi yameandikwa au kunukuliwa katika habari (magazetini, redioni na kwenye vipindi vya luninga) zaidi ya mara 1000 huku ikipata ushiriki na mjadala zaidi ya milioni kwenye mitandao ya kijamii.

Hizi ni program kubwa tatu zinazotekelezwa kwa miaka mingi na shirika la Twaweza. Kwa kuongezea, tunaendesha na kushiriki katika miradi kadhaa midogo midogo na ya muda mfupi zaidi ya mia moja ambayo yote inabuniwa kwa kusudi kubwa la kujenga na kupanua mahusiano mapana na yenye tija baina ya wananchi na serikali zao.

Bongo5
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad