Ligi kuu ya soka Tanzania bara msimu wa 2018/19 inatarajiwa kuanza bila kuwepo kwa mdhamini mkuu kutokana na pande mbili ambazo ni Shirikisho la soka nchini TFF na wadhaini waliowasilisha ofa kutofikia muafaka mpaka sasa.
Akiongea na www.eatv.tv mtendaji mkuu wa bodi ya ligi Boniface Wambura amethibitisha kuwa ligi hiyo itaanza bila mdhamini mkuu huku akiweka wazi kuwa maongezi na makampuni mbalimbali yaliyoomba kudhamini ligi kuu kwa msimu ujao hayajakamilika.
''Kalenda ya mashindano imeshafika na ligi inatakiwa kuanza hatuwezi kusubiri mdhamini, akipatikana ataingia wakati ligi inaendelea ila kwasasa tutakuwa na wadhamini wengine wadogo kama tulivyowatangaza'', amesema.
Ligi kuu soka Tanzania bara imekuwa chini ya udhamini wa kampuni ya simu ya Vodacom kwa miaka kadhaa lakini mpaka sasa kampuni hiyo na TFF hawajafikia makubaliano juu ya kuendelea au kutoendelea. Hivi karibuni TFF ilisaini mkataba na Benki ya KCB kama moja ya wadhamini wa ligi msimu ujao kwa dau la milioni 420.
Ligi hiyo inatarajia kuzinduliwa Jumamosi hii, Agosti 18 kwa mechi ya Ngao ya jamii itakayowakutanisha mabingwa Simba SC na mabingwa wa kombe la shirikisho Mtibwa Sugar mchezo ambao utapigwa kwenye uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Ligi yenyewe rasmi itaanza Agosti 22 kwa mchezo wa ufunguzi kati ya Simba SC dhidi ya Tanzania Prison ya Mbeya. Yanga wao watafungua msimu Agosti 23, ugenini dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye uwanja wa Jamhuri Morogoro.