MWENYEKITI wa Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Sadick Murad, amesema wanatarajia kukutana na serikali kutafuta mwafaka wa upatikanaji wa saruji hususan iliyokwama njiani kutokana na zuio lililowekwa.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira, Sadick Murad (katikati), akizungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana, kuhusu mafanikio na changamoto mbalimbali walizokutana nazo baada ya ziara yao ya kutembelea viwanda zaidi ya 12 katika Mkoa wa Dar, iliyoratibiwa na Shirikisho la wenye Viwanda Tanzania (CTI).
Murad aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akihojiwa na waandishi wa habari baada ya kutoa taarifa ya ziara iliyofanywa na kamati yake.
Alisema kamati itazungumza na serikali kuhusu saruji iliyokuwa njiani kwenda nje ya nchi ili kuona namna ya kuwasaidia wasafirishaji wa bidhaa hiyo wasipate hasara.
Alisema lengo la serikali kuzuia saruji hiyo kupelekwa nje ya nchi halikuwa na nia mbaya kwani inataka kutosheleza kwanza mahitaji ya ndani ndipo iruhusu kusafirisha nje ya nchi.
“Saruji itaruhusiwa kwenda nje iwapo mahitaji ya ndani yatajitosheleza. Tusije tukaanza kutafuta saruji kutoka nje ya nchi kukidhi mahitaji ya ndani wakati sisi wenyewe tunaweza kuzalisha ya kutosha,” alisema
Alisema kutokana na uhaba ambao ulijitokeza, serikali imetaka viwanda vyote vijitosheleze mahitaji ya ndani baada ya hapo itaruhisiwa kusafiri kwa kuwa hilo zuio sio la kudumu.
Aidha, alisema wakati wakiwa kwenye ziara walijulishwa kuwa viwanda vya saruji vitatu vilifanya matengenezo kwa wakati mmoja na kusababisha uzalishaji kupungua.
“Pia viwanda vililalamika kuwa havina magari ya kutosha ya kwenda kuchukua makaa, hivyo makaa hayaji kwa wakati na wenye magari wakasema hawana mkataba na wenye viwanda,” alisema Murad.
Alisema baadhi ya wenye viwanda walikuwa wanataka wapatiwe vibali ili waagize makaa kutoka nchini Afrika Kusini kwasababu hawakutaka kutumia makaa ya Tanzania.
Murad alisema tayari serikali ilikutana na wenye viwanda kwa ajili ya kuzungumza nao na huenda wakawa wamefikia suluhu.
Wiki hii serikali ilizuia saruji kusafirishwa nje ya nchi kutokana na uhaba wa bidhaa hiyo ambayo ilisababisha mfuko mmoja wa saruji kuuzwa hadi Sh. 18,000.