Shirikisho la kandanda nchini Uingereza, FA lipo katika mipango ya kuomba nafasi ya kuandaa michuano ya kombe la dunia mwaka 2030.
Kupitia kwa mwenyekiti wa chama hicho, Creg Clarke ambaye amethibitisha kuwa bodi ya chama hicho imefikia makubaliano ya kuanza kazi hiyo kuona kama itawezekana.
"Kazi hiyo itaanza rasmi katika msimu huu mpya na kwamba hakuna maamuzi yoyote yatakayofanyika hadi mwaka 2019". Ameongeza mwenyekiti huyo.
Michuano ya mwisho mikubwa ya soka kufanyika nchini Uingereza ni ya mwaka 1996 ambayo ni michuano ya mataifa ya ulaya, bingwa wa michuano hiyo akiwa ni Ujerumani baada ya kuifunga jamhuri ya Czech.
Ilishindwa kupata nafasi ya kuandaa michuano ya kombe la dunia ya mwaka 2018 iliyomalizika nchini Urusi, ambapo sasa ina imani kubwa ya kufanikisha azma hiyo kutokana na uwazi wa zoezi la upigaji kura lililofanyika hivi karibuni ambalo lilizipa tiketi nchi za Marekani, Mexico na Canada kwa pamoja kuandaa michuano ya mwaka 2026.
Nchi hyo pia inatarajia kupata upinzani kutoka kwa mataifa ya Argentina, Uruguay na Paraguay ambayo yanapanga kuomba nafasi ya kuandaa michuano hiyo kwaajili ya kuadhimisha miaka 100 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1930.
Uingereza ina historia ya kushinda kombe la dunia mara moja mwaka 1966, michuano iliyofanyika katika ardhi ya nyumbani ambapo ilishinda kwa penalti 4-2 dhidi ya Ujerumani magharibi ambayo baadaye iliungana na Ujerumani mashariki na kuwa nchi moja.