Msanii wa Bongo Fleva Mwasiti Almasi, amefunguka na kudai umri wake hauwezi kuwa tatizo la yeye kutokuendelea kujihusisha na masuala ya muziki kwa kuwa ana imani bado ana uwezo mkubwa wa kuitendea haki sanaa.
Mwasiti ametoa kauli hiyo kwenye kipindi cha Planet Bongo kinachorushwa na East Africa Radio leo Agosti 15, muda mchache alipomaliza kutambulisha wimbo wake mpya wa 'Mapene' ulioandikwa na Marioo kwa kushirikiana na yeye mwenyewe huku ukitayarishwa na Kimambo.
"Sijawahi kukata tamaa na muziki, bado nina uwezo wa kuufanya. Toka nimeanza muziki naweza kusema nimeweza kutimiza zaidi ya asilimia 60 ya malengo yangu. Umri sio tatizo katika kufanya kazi maana hata ukimuangalia Joseph Haule 'Prof. Jay' ni Mbunge lakini 'still' anaendelea kufanya muziki", amesema Mwasiti.
Pamoja na hayo, Mwasiti ameendelea kwa kusema "hata nje ya nchi kuna wasanii wenye umri mkubwa lakini huwasikii wameacha kufanya kazi, licha ya kuwa kuna umri ukifika huwezi kuendelea kuonekana juu ya majukwaa kufanya show".
Kauli hizo za Mwasiti zimekuja baada ya wadau wengi kuamini vichwani mwao, kuwa wasanii wa zamani hawana uwezo wa kuendelea kimuziki katika nyakati za sasa, kutokana na kuwepo wimbi kubwa la wasanii chipukizi na kubadilika soko la kibiashara.