Taifa la Korea Kaskazini halijasitisha mpango wake wa kinyuklia pamoja na ule wa kutenegeneza silaha , hivyobasi kukiuka vikwazo vya Umoja wa Mataifa , kulingana na ripoti iliotolewa na baraza la usalama la Umoja wa mataifa.
Ripoti hiyo inasema kuwa Pyongyang imeongeza idadi ya meli zinazosafirisha bidhaa za mafuta na imekuwa ikijaribu kuuza silaha ng'ambo.
Ripoti hiyo ya siri ilioandaliwa na jopo la wataalam iliwasilishwa kwa baraza la usalama la umoja wa mataifa siku ya Ijumaa.
Korea Kaskazini hadi kufikia sasa haijatoa tamko lolote kuhusu ripoti hiyo.
Wiki iliopita maafisa wa Marekani walisema kuwa Pyongyang ilikuwa ikitengeneza silaha za masafa marefu licha ya mkutano wa kufana na rais wa Marekani Donald Trump ambapo iliahidi kufutilia mbali mipango yake yote ya kinyuklia.
Afisa mmoja ambaye hakutajwa jina aliambia gazeti la The Washington Post kwamba setlaiti za upelelezi ziligundua kwamba kuna maswala yaliokuwa yakiendelea katika kituo ambacho kilikuwa kikiunda silaha za masafa marefu.
Rais Donald Trump alikutana na rais Kim Jong Un nchini Singapore mnamo mwezi Juni na viongozi hao waliahidi kufanya kazi pamoja kwa lengo la kusitisha mipango ya kinyuklia bila kuelezea kuwa ni hatua gani zitakazofuatwa.
UN: Korea Kaskazini Inaendelea na Mpango Wake wa Kinyuklia
0
August 04, 2018
Tags