Ushindi wa Yanga Wazipambanisha Timu za Kundi D

Ushindi wa Yanga Wazipambanisha Timu za Kundi DWawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya kombe la shirikisho klabu ya Yanga, jana imepata ushindi wake wa kwanza kwenye kundi D, wa mabao 2-1 dhidi ya USM Alger ya Algeria na kuzifanya timu 3 katika kundi hilo zigombanie nafasi ya kwenda robo fainali.

Yanga tayari imeshatupwa nje ya michuano hiyo ikiwa na alama 4 tu kwenye mechi 5 za kundi D lenye timu za Gor Mahia yenye alama 8 kileleni, USM Alger yenye alama 8 katika nafasi ya pili na Rayon Sports yenye alama 6 katika nafasi ya tatu. Kimahesabu timu zote tatu za juu zina nafasi ya kufuzu hatua ya robo fainali.

Kuelekea kwenye mechi za mwisho za makundi, vinara Gor Mahia wao watasafiri kwenda nchini Algeria kusaka sare au ushindi dhidi ya wenyeji wao USM Alger ili wajihakikishie kusonga mbele. Wakati huo USM Alger naye anasaka matokeo kama ya Gor Mahia ili aweze kuwa miongoni mwa timu mbili zitakazocheza robo fainali kutoka kundi D.

Wakati USM Alger na Gor Mahia wakikipiga, Rayon Sports ambao wana alama 6 watakuwa nyumbani wakisaka ushindi dhidi ya Yanga na endapo watashinda watafikisha alama 9 na kusubiri matokeo ya Gor Mahia na USM Alger. Endapo Gor Mahia itatoa sare na USM Alger huku Rayon Sports ikishinda dhidi ya Yanga timu zote tatu zitafikisha alama 9 na tofauti ya magoli ya kufunga na kufungwa ndio itaamua timu gani iende.

Safari ya Yanga SC katika michuano hiyo ilianza kwa kuchapwa mabao 4-0 na U.S.M. Alger nchini Algeria kabla ya kuja kutoa sare ya 0-0 na Rayon jijini Dar es Salaam na baadaye kufungwa na Gor Mahia 4-0 nchini Kenya na 3-2 waliporudiana hapa nchini kabla ya jana usiku kupata ushindi dhidi ya USM Alger kwenye uwanja wa taifa.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad