Mwigizaji maarufu nchini Irene Uwoya amesema anajuta kutokwenda kumjulia hali marehemu Amri Athuman maarufu Mzee Majuto alipokuwa amelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Uwoya ameileleza MCL Digital leo Ijumaa Agosti 10, 2018 kuwa Mzee Majuto alipokuwa akipatiwa matibabu hospitalini hapo, alimuita aende kumuona.
Majuto alifariki dunia Agosti 8, 2018 akiwa anapatiwa matibabu katika hospitali. Anatarajiwa kuzikwa leo kijijini kwake Kiruku mkoani Tanga.
Akizungumzia msiba wa nguli huyo wa vichekesho nchini, Uwoya amesema ameacha pengo kubwa katika tasnia ya uigizaji na Taifa.
Amesema kinachomsikitisha zaidi ni kutokwenda kumjulia hali Majuto, “yaani naumia na wala sijui nielezeje, mbaya zaidi hata pale alipokuwa akiumwa na kulazwa hospitali kwa nyakati tofauti nilishindwa kwenda kumuona pamoja na kwamba alishanipigia simu mara mbili niende lakini sikufanya hivyo.”
“Nilikuwa na majukumu mengi kwa kweli na kuna kipindi nilikuwa na nafasi lakini sijui nini kilichokuwa kinanifanya nishindwe kwenda, hii kitu itaendelea kuniumiza kwakweli.”
Akimzungumzia namna walivyoishi na Majuto, amesema alikuwa ni zaidi ya msanii na walimchukulia kama baba yao, babu yao na yeye alishaenda hadi nyumbani kwake Tanga.
Amesema marehemu atakumbukwa kwa kutopenda kujikweza na kuheshimu mashabiki na watu wengine.