VIGOGO tisa wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) akiwemo Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe wamewasilisha maombi ya kutaka kesi hiyo iahirishwe mpaka rufaa yao itakaposikilizwa na kutolewa maamuzi.
Maombi hayo yamewasilishwa leo Agosti 13, mwaka huu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na wakili wa utetezi, Jeremiah Mtobesya mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Wilbard Mashauri.
Katika maombi yao, upande wa utetezi unaomba mahakama ya Kisutu kuahirisha kesi hiyo mpaka hapo rufaa yao waliyofungua mahakama ya Rufani itakaposikilizwa na kutolewa maamuzi.
Washtakiwa hao walikata rufaa kupiga maamuzi ya Mahakama kuu yaliyotolewa mwezi uliopita ambayo yalitupilia mbali maombi yao ya kutaka kesi hiyo ifanyiwe marejeo juu ya uamuzi mdogo uliotolewa na mahakama ya Kisutu.
Wakili wa Serikali Mkuu, Zainabu Mango amesema wamepokea hati ya maombi hayo namba 10.2018 na kwamba wapo tayari kuwasilisha majibu kinzani kesho Agosti 14.
Wakili wa utetezi, Mtobesya ameomba wapewe muda wa siku mbili hadi Agosti 16 ili waweze kufaili majibu ya nyongeza kama watakuwa nayo.
Baada ya kusikiliza pande zote mbili, Hakimu Mashauri ameamuru upande wa mashtaka kuwasilisha majibu kinzani Agosti 14.mwaka huu na kama upande wa utetezi watakuwa na majibu ya nyongeza wayawasilishe Agosti 21, mwaka huu.
Maombi hayo yatasikilizwa Agosti 21, mwaka huu na kesi ya msingi nayo pia itatajwa Agosti 21 mwaka huu.
Washitakiwa wengine kwenye kesi hiyo ni Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Vincent Mashinji, Mbunge wa Iringa Mjini Msigwa, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu na Naibu katibu Mkuu bara na Mbunge wa Kibamba, John Mnyika na wengine wanne.
Wote kwa pamoja wanakabiliwa na kesi ya uchochezi.
Vigogo Chadema Wawasilisha Maombi ya Kusimamisha Kesi Mpaka Rufaa Yao Isikilizwe
0
August 13, 2018
Tags