Jaji Koroso aliyesikiliza maombi hayo, anatoka Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, Kitengo cha Makosa ya Uhujumu Uchumi na Rushwa maarufu kama Mahakama ya Mafisadi.
Mahakama hiyo iliketi kwa siku mbili na kutoa uamuzi wake jana, baada ya mawakili wa upande wa utetezi ambao wanawawakilisha washtakiwa hao kuweka pingamizi, wakidai kwamba kuna udhaifu katika hati iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP).
Wanaokabiliwa na kesi hizo ni Mwenyekiti wa zamani wa Chama Kikuu cha Ushirika mkoani humo (KNCU 1984 Ltd), Aloyce Kitau, makamu wake, Hatibu Mwanga na Katibu Mkuu, Honest Temba. Wote kwa pamoja wanatuhumiwa kuusababishia ushirika huo hasara ya Sh. bilioni 2.9
Wengine ni aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Kiwanda cha Kukoboa Kahawa cha Tanganyika Coffee Curing Co. Ltd (TCCCo), Meynard Swai na Meneja Mkuu wa kiwanda hicho, Andrew Kleruu, ambao wanadaiwa kukisababishia hasara ya Sh. bilioni 1.6
Akisoma uamuzi huo jana, Jaji Koroso alisema mahakama hiyo imepima kwa umakini maombi ya dhamana hiyo na imeona hayana msingi, kwa kuwa suala hilo linagusa maslahi ya wanachama wa KNCU.
Jaji huyo alisema katika hati za viapo vya dhamana zilizowasilishwa katika mahakama hiyo, ni dhahiri kwamba si halali kisheria kwa sababu zimewasilishwa zikiwa zimedurufiwa na si halisi.
Katika shtaka la kwanza, Kitau (70), Mwanga (70) na Temba (38) wanatuhumiwa kwa matumizi mabaya ya ofisi kinyume cha kifungu cha 96 (1) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 ya Sheria iliyofanyiwa Marejeo Mwaka 2002.
Ilidaiwa katika tarehe tofauti, kati ya Julai, 2014 na Novemba, 2017 wakiwa katika Manispaa ya Moshi, Kilimanjaro, walitumia vibaya mamlaka ya ofisi yao na bila kufuata sheria, kuilipa fidia Kampuni ya Ocean Link Shipping Services Ltd.
Shitaka la pili ambalo pia linawakabili washtakiwa wote watatu, ni la kuisababishia hasara KNCU, kinyume cha Aya ya 10 (1) cha Jedwali, na vifungu vya 57 na 60 (2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi, Sura ya 200 ya Sheria iliyofanyiwa Marejeo Mwaka 2002.
Swai (57) na Kleruu (56) kwa upande wao, kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka mawili ya matumizi mabaya ya ofisi, kinyume na kifungu cha 96 (1) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa Marejeo Mwaka 2002 na la pili ni la kukisababishia hasara kiwanda hicho.