Zoezi la vipimo vya kuhakiki umri wa wachezaji wa timu shiriki kuelekea michuano ya kufuzu fainali za AFCON za vijana U-17 kanda ya Afrika Mashariki limekamilika huku wachezaji kadhaa waliozidi umri ‘Vijeba’ wakinaswa.
Madaktari wakimfanyia vipimo mchezaji wa timu ya Taifa ya Vijana ya Tanzania U17”Serengeti Boys” Ben Anthony Starkie anayecheza Leicester City U16 ya England.
Katika zoezi hilo lililofanyika katika hospitali ya taifa ya Muhimbili likisimamiwa na madaktari wa Shirikisho la soka barani Afrika CAF.
Miongoni walionaswa katika vipimo hivyo ni wachezaji wawili wa timu ya taifa ya vijana ya Tanzania, Serengeti Boys, Jafary Mtoo na Lenox Fred ambao wamethibitika kuzidi umri wa miaka 17.
Kwa mujibu wa taarifa ya Makamu wa Rais wa kamati ya tiba ya CAF, Dk Yacine Zerguini imewataja wachezaji wengine walioenguliwa ni Abdoul Intwari wa Burundi, Maxwell Mulili, Lesley Otieno na Abdulmalik Hussein Abdallah wa Kenya.
Wengine ni Simon Pitia Alberto wa Sudan Kusini, Gamel Abdul Kamal wa Sudan, Oluka George, Kafumbe Joseph na Elvis Ngonde wa Uganda.
Michuano hiyo ya vijana ya kufuzu AFCON 2018 kanda ya CECAFA inaanza leo Jijini Dar es Salaam kwa mchezo wa mapema kati ya Rwanda na Sudan na baadaye wenyeji Tanzania watamenyana na Burundi huku kiingilio kikiwa ni bure.