Vitisho Vyamfanya Meya Ilala Kupitia CUF Omary Kumbilamoto Kujiuzulu

Vitisho Vyamfanya Meya Ilala Kupitia CUF Omary Kumbilamoto  Kujiuzulu
Diwani wa Kata ya Vingunguti ambaye pia ni Naibu Meya wa Ilala, Omary Kumbilamoto (CUF) amejiuzulu nyadhfa zake asubuhi hii huku akidai sababu kubwa ya yeye kuchukua maamuzi hayo ni kutokana na migogoro iliyopo ndani ya chama chake.

Kumbilamoto ameeleza hayo wakati alipokua anazungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo asubuhi Agosti mosi, 2018 na kusema sababu kubwa ya yeye kufanya hivyo, ni kutokana na kutishwa na viongozi wa chama hicho, pindi anapokuwa anaungana na viongozi wa serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo.

"Kuanzia leo najiuzulu nafasi yangu ya udiwani wa kata ya Vingunguti pamoja na ya unaibu Meya wa Ilala, hivyo sasa mimi ni mtu huru. Nitaelekea kufanya mambo yangu ya kilimo lakini hapo baadae nitawaambia wananchi wangu ni chama gani ambacho nitajiunga nacho", amesema Kumbilamoto.

Pamoja na hayo, Kumbilamoto ameendelea kwa kusema "nina mpongeza Rais Magufuli kwa kuweza kurudisha watumishi wa umma katika mstari unaohitajika, ambapo mambo hayo sisi tulikuwa wasafiri tulikuwa tunayaona kwa wenzetu lakini hivi sasa Rais Magufuli ameweza kuyarudisha na nchini kwetu".

Akizungumza na www.eatv.tv Mwenyekiti wa chama hicho Wilaya ya Ilala, Bakari Shingo amesema wamesikia taarifa za kujiuzulu diwani wao huku akisikitika juu ya madai yaliyomfanya kung'atuka ndani ya CUF.

"Siku zote migogoro ndani ya chama ni jambo la kawaida ila ninachoamini ameafuata upepo tu wa kisiasa. Mimi nasema waache waondoke na upinzani hautaweza kufa. Kila diwani anayetaka kuondoka na aondoke sisi tutaendelea kubaki kwenye msimamo wetu na taifa kiujumla", amesema Shingo.

Wakati vuguvugu la kisiasa likiwa linaendelea hasa katika upande wa upinzani kuhama vyama vyao na kuenda kuunga mkono jitihada za Rais Magufuli katika ujenzi wa taifa, wachambuzi mbalimbali wa siasa, wamesema suala hilo ni jambo la kawaida kutokea kwa madai hiyo ni haki ya kila mtu kuchagua chaguo sahihi.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad