Aliyekuwa Mbunge wa Ukonga kwa tiketi ya Chadema kabla ya kuhamia CCM, Mwita Waitara amesema suala la gharama za kurudia uchaguzi halimhusu bali anachotaka ni kuhakikishiwa ubunge wake.
Akizungumza katika mahojiano na Mwananchi leo Agosti 15, Waitara amesema ameamua kuhama baada ya kuona nafasi yake ya ubunge inatishiwa kutokana na kudorora kwa uhusiano kati yake na Mwenyekiiti wa Chadema, Freeman Mbowe.
Hata hivyo, Mbowe alipotafutwa kwa njia ya simu kujibu kauli hiyo, amesema hawezi kuzungumza kwa kuwa yuko kwenye kikao cha kamati kuu ya chama hicho.
Awali Waitara alipotangaza kuondoka Chadema Julai 28, Mbowe aliliambia Mwananchi kuwa hakuwahi kumzuia kugombea uenyekiti wala kuwa na ugomvi naye.
“Sitegemei mtu akiondoka Chadema akamsifu Mbowe, lazima atarusha mawe kwenye mti wenye matunda,” alikaririwa Mbowe.