Wakili Afunguka Kilichomwondoa Katika Kesi ya Mbowe na Wenzake

Wakili Afunguka Kilichomwondoa Katika Kesi ya Mbowe na Wenzake
Wakili Jeremiah Mtobesya amejitoa kuwawakilisha katika kesi viongozi tisa wa Chadema, akiwamo mwenyekiti Freeman Mbowe akisema anaona haki haitatendeka.

Mtobesya alijiondoa katika kesi hiyo iliyopo Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri.

Alifikia uamuzi huo baada ya Mahakama kutoa uamuzi wa kutupilia mbali maombi ya wateja wake ya kutaka kesi hiyo ya jinai namba 112/2018 iahirishwe ili kusubiri kusikilizwa maombi na rufani iliyopo Mahakama ya Rufaa.

Washtakiwa wamewasilisha katika Mahakama ya Rufaa maombi wakitaka kesi ya msingi iliyopo Kisutu isitishwe usikilizwaji hadi rufaa ya kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu wa kutupilia mbali maombi ya marejeo namba 126/2018 itakaposikilizwa na uamuzi kutolewa.

Katika Mahakama Kuu, washtakiwa waliiomba irejee mwenendo wa kesi na uamuzi uliotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Jana, baada ya Hakimu Mashauri kuyatupilia mbali maombi ya washtakiwa aliamuru wasomewe maelezo ya awali ya kesi inayowakabili.

Wakili Mtobesya alieleza kuwa kesi ilipangwa kwa ajili ya kutajwa na uamuzi ulitolewa.

Alisema hakubaliani na ombi la upande wa mashtaka la kuwasomea washtakiwa maelezo ya awali.

Wakili Mtobesya aliieleza Mahakama kuwa anajiondoa katika kesi kwa sababu anaona kwa namna mwenendo wa kesi unavyokwenda haki haitatendeka.

Kwa kauli hiyo, Mtobesya alibeba begi lake na kuondoka ndani ya ukumbi namba moja wa Mahakama ambako kesi ilikuwa ikiendeshwa.

Aliwaacha washtakiwa wakiwa hawana wakili mahakamani kwa kuwa wakili mwingine anayewawakilisha, Peter Kibatala hakuwapo.

Hakimu Mashauri aliwaeleza washtakiwa kwa kuwa hawakuwa na wakili mwingine mahakamani, anaahirisha kesi hadi Agosti 27 watakaposomewa maelezo ya awali.

Sababu za maombi kutupwa

Hakimu Mashauri katika uamuzi wa kutupilia mbali maombi ya washtakiwa, alisema kifungu cha sheria ya mwenendo wa mashauri ya jinai kilichotumika kuwasilisha maombi hayo, hakiipi Mahakama mamlaka ya kuahirisha kesi kusubiri uamuzi wa Mahakama ya Rufaa.

Alisema hata kama kifungu hicho kingekuwa kinaipa Mahakama mamlaka ya kufanya hivyo, basi isingefanya hivyo kwa sababu ilishatoa uamuzi mara kadhaa kutokana na maombi mbalimbali ya utetezi na kuyatupilia mbali, hivyo haiwezi kula matapishi yake.

Baada ya uamuzi kutolewa, wakili wa Serikali mkuu, Faraja Nchimbi alisema kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kutajwa, na kwa kuwa uamuzi umeshatolewa aliiomba Mahakama iridhie washtakiwa wasomewe maelezo ya awali. Ombi hilo lilipingwa na Mtobesya.

Hakimu Mashauri alisema ni kweli kesi ilipangwa kwa ajili ya kutajwa kusubiri uamuzi ambao alishautoa, hivyo haoni haja ya kuahirisha kusomwa kwa maelezo ya awali.

Alisema usomaji wa maelezo hayo hauhitaji maandalizi, hivyo aliamuru upande wa mashtaka kuwasomea washtakiwa hao.

Wakili Kibatala alipowasilisha maombi awali, alidai Mahakama hiyo ina mamlaka ya kuiahirisha kesi ya jinai namba 112/2018 kwa kipindi kisichozidi siku 15 iwapo mshtakiwa atakuwa ndani na kisichozidi siku 30 iwapo mshtakiwa au washtakiwa watakuwa nje kwa dhamana.

Wakili Nchimbi alidai kuwa maombi hayo ya utetezi yanakosa baraka za kisheria na hata miguu ya kisheria ya kusimama mbele ya Mahakama hiyo.

Aliiomba Mahakama itupilie mbali maombi yaliyowasilishwa na upande wa utetezi kwa sababu yanakosa msingi wa kisheria.

Alidai maombi ya upande wa utetezi yanalenga kuchelewesha kesi na hakuna kipya kilichowasilishwa mahakamani. Mbali na Mbowe washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya jinai ni naibu katibu mkuu wa Chadema –Zanzibar, Salum Mwalimu na naibu katibu mkuu –Bara, John Mnyika ambaye pia ni mbunge wa Kibamba.

Wengine ni wabunge wa Tarime Vijijini, John Heche; Halima Mdee (Kawe), Ester Bulaya (Bunda), Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini), Esther Matiko (Tarime Mjini) na katibu mkuu wa chama hicho, Dk Vincent Mashinji.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji jinai.

Washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Februari Mosi na Februari 16 jijini Dar es Salaam.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad