Wakili wa kimataifa aliyekuwa amepewa kazi ya kumwakilisha mbunge wa Kyadondo Mashariki Robert Kyagulanyi, maarufu kama Bobi Wine, amezuiwa kuingia nchini humo, taarifa zinasema.
Gazeti la kibinafsi la the Monitor nchini humo limeripoti kuwa Robert Amsterdam ameorodheshwa kama mtu asiyetakikana nchini Uganda na serikali ya nchi hiyo.
Alikuwa miongoni mwa mawakili waliokuwa wameorodheshwa kumtetea Bw Kyagulanyi katika kesi ambapo ameshtakiwa uhaini.
Jukumu la Bw Amsterdam lilikuwa kufanya masuala ya kiufundi, kutoa ushauri na pia kusaidia katika kufanya utafiti.
Wakili huyo ni raia wa Canada lakini huendesha shughuli zake kupitia kampuni ya Amsterdam & Partners iliyo na afisi Washington na London.
Bobi Wine amekuwa akizuiliwa rumande katika gereza la Gulu pamoja na watuhumiwa wengine 33, miongoni mwao wabunge.
Anadaiwa kuhusika katika kurushia mawe magari ya msafara wa Rais Yoweri Museveni wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa eneo bunge la Arua.
Kassiano Wadri aliyeshinda ubunge Arua ni miongoni mwa wabunge waliozuiliwa.
Maafisa wakuu wa serikali Uganda kufikia sasa bado hawajazungumzia taarifa hizo.
Bw Medard Sseggona, mmoja wa mawakili Kyagulanyi amesema hatua ya kumzuia Bw Amsterdam kuingia nchini humo si ya busara, na inaweza tu kuashiria kwamba serikali imeanzakuingiwa na wasiwasi.
Bw Amsterdam katika makala iliyochapishwa kwenye vyombo vya habari Uingereza Jumamosi alikuwa amezungumzia kukamatwa na kuzuiliwa kwa wabunge Uganda na kimya cha jamii ya kimataifa.
Kwenye gazeti la The Guardian, alitoa wito kwa jamii ya kimataifa kuwawekea vikwazo watu wanaohusika katika ukiukaji wa haki za kibinadamu nchini Uganda.
"Vikwazo kama hivi vinaweza kufanikiwa vyema katika kuzuia ukiukaji wa haki za kibinadamu siku za usoni, na kuzuia madhara zaidi kwa raia wasio na hatia," aliandika.