WAKATI kocha wa Simba, Mbelgiji Patrick Aussems, akiwataka mashabiki wa klabu hiyo kufika kwa wingi Uwanja wa Taifa kushuhudia kazi aliyoifanya kwa wiki mbili nchini Uturuki, wapinzani wao Asante Kotoko wametaja silaha zao 18 zitakazowavaa leo.
Asante Kotoko ambao walitua jana jijini Dar es Salaam, wamekuja na jumla ya wachezaji 18 miongoni mwao wakiwamo makipa wawili Felix Annan, Kwame Osei
Mabeki ni Amos Frimpong, Augustine Sefa, Samuel Appiah Kubi, Wahab Adams, Nafiu Awudu, Emmanuel Owusu na Agyemang Badu.
Kwa upande wa viungo ni Akwasi Nti, Jordan Opoku, Prince Acquah, Douglas Owusu Ansah na Micheal Yeboah.
Mastraika ni Osman Ibrahim , Sougne Yacouba, Obed Owusu na Frederick Boateng.
Kocha wa Simba, Aussems, alisema mchezo huo wa kilele cha maadhimisho ya Tamasha la Simba Day, ni kipimo kizuri kwao kwa kuwa wanacheza na timu kubwa Afrika.
“Tumefanya maandalizi ya kutosha… mchezo wa kesho [leo] ni kipimo kizuri kwetu kuangalia nini tumefanikiwa…, utakuwa mchezo mzuri na mashabiki waje kwa wingi,” alisema.
Alisema ameridhika na maandalizi ya timu yake na sasa watawaonyesha mashabiki kile walichokifuata Uturuki.
Aussems alisema wachezaji wake wote wapo kwenye hamasa ya kutaka kuonyesha kitu kwa mashabiki wao.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa timu hiyo, Haji Manara, alisema milango itaanza kufunguliwa majira ya saa 2:00 asubuhi.
Msaga Sumu, Mwasiti Tunda Man kunogesha
Katika hatua nyingine, Manara alisema ili kulifanya tamasha hilo kuwa la mvuto wa aina yake na burudani ya kutosha, wanamuziki Msaga Sumu, Mwasiti na Tundaman watakuwa sehemu ya burudani kwa mashabiki watakaohudhuria.
Alisema wasanii hao wataanza kutoa burudani kabla ya kuanza kwa mchezo wa timu ya Simba B dhidi ya Dodoma FC na kisha Simba na Asante Kotoko.
Aidha, Manara alitoa tahadhari kwa watu wenye nia ya kulangua tiketi watakutana na rungu la polisi.
“Ulinzi utakuwa wa hali ya juu, naomba kuwafahamisha wale wanaopanga kuja kulangua tiketi au kufanya vitu vya aina yoyote vya tofauti.., kutakuwa na ulinzi wa kutosha hivyo wasijidanganye, watadhalilika,’ alisema Manara.