Wanaume kupimwa UKIMWI usiku

Wanaume kupimwa UKIMWI usiku
Mkuu wa wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga Anamringi Macha, amesema wana mpango wa kuanzisha huduma za upimaji wa virusi vya UKIMWI (VVU) na huduma ya uchangiaji damu kwa hiari nyakati za usiku kutokana na wanaume wengi kujitokeza kwa wingi muda huo.


Ameyasema hayo wakati akitoa taarifa ya huduma ya upimaji wa virusi vya UKIMWI, malaria na huduma ya kuchangia damu kwa hiari, ambapo ameweka wazi kuwa asilimia kubwa ya wanaojitokeza mchana kupima VVU ni wanawake ukilinganisha na wanaume.

''Tuna mpango wa kuanza kutoa huduma hiyo nyakati za usiku kuanzia saa moja jioni na kuendelea hali ambayo itasaidia wanaume ambao wanaogopa kujitokeza mchana  kujitokeza usiku kupima virusi vya Ukimwi, malaria pamoja na kuchangia damu kwa hiari'', alisema.

Katika taarifa yake Mh. Macha ameeleza, waliojitokeza kupima virusi vya UKIMWI katika mkesha wa mbio za Mwenge wilayani humo walikuwa 655,  wanaume wakiwa 537 na wanawake118. Waliochangia damu kwa hiari walikuwa 108, wanaume 94 na wanawake 14.

Alisema waliojitokeza kupima malaria walikuwa 12 na waliokutwa na malaria alikuwa mmoja na kuwataka wananchi kuwa na desturi ya kulala ndani ya vyandarua na kufukia madimbwi ya maji machafu ili mbu wasiendelee kuzaliana na kueneza ugonjwa.

Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Kahama, Lucas Ngamtwa, alisema kuna mradi wa furaha yangu Kitaifa ambao unatoa huduma ya kupima VVU usiku kuanzia saa moja jioni  na kuwa mradi huo utaendelezwa na Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Kahama baada ya kufika kikomo.


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad