Kama una desturi ya kutembea bila kitambulisho chako cha Uraia na ni mkazi wa Jiji la Dodoma basi acha mara moja tabia hiyo kwani Jeshi la Polisi Mkoani humo limeanza mchakato wa kuwahoji watu wote watakaokamatwa hawana vitambulisho vya Uraia.
Kauli hiyo imetolewa jana Agosti 7, 2018 na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Bilinith Mahenge ambapo ameagiza wakazi wa Dodoma kutii agizo hilo kwani limeanza kutekelezwa huku akiwataka watu ambao vitambulisho hivyo kwenda mara moja NIDA kushughulikia mchakato wa kuvipata.
“Sasa niwaombe wananchi wa Dodoma na maeneo mengine, kwamba sisi tutafanya msako tunataka Dodoma pawe salama. Na ni vizuri Kuanzia sasa nimeongea na NIDA kwamba zoezi la kutoa vitambulisho vya uraia linaisha mwezi Desemba mwaka huu, tutataka kila atakayekuwa na kitambulisho atembee nacho, ndio utambulisho wake, tutakuhoji kwa kitambulisho chako. Na ni practice ya dunia nzima.“amesema Mahenge.
Kwa upande mwingine, RC Mahenge amesema mpango huo wa serikali mkoani Dodoma ni moja ya mikakati ya kuimarisha ulinzi na Usalama wa jiji la Dodoma kutaka kuwa jiji la mfano Tanzania.