Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam inawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kuteka watu na kudai fedha kiasi cha Sh60 milioni kwa ndugu wa waliotekwa.
Watuhumiwa ni Mkazi wa Kimara Mwisho Hussein Shilingi (30) na mkazi wa Tabata Martine Pumba(35).
Watuhumiwa wote walikamatwa Julai 26 mwaka huu maeneo ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) wakitumia gari aina ya Toyota Land Cruiser yenye namba ya Umoja wa Mataifa (UN) huku wakiwa na watu watano waliowateka.
Kamanda wa Polisi kanda hiyo Lazaro Mambosasa akizungumza jana Agosti 3 amesema baada ya kufanya upekuzi ndani ya gari hilo walifanikiwa kukamata vifaa mbalimbali vilivyokuwa vikitumiwa na wahalifu hao ikiwamo namba za magari za mashirika ya serikali, Umoja wa Mataifa na namba za binafsi.
Mambosasa amesema baada ya kuhojiwa, waliotekwa walisema walitekwa kuanzia 23 Julai hadi 25 mwaka huu.
Amesema walitakiwa kutoa Sh60milioni ambapo watekaji hao walikuwa wanatumia mbinu ya kupiga simu kwa ndugu waliotekwa na kudai fedha hizo ili wawaachie huru.
“Hawa watekaji walikuwa wanatumia gari moja lakini walikuwa wanabadilisha namba tofauti za magari kama za serikali, ubalozi na za umoja wa kimataifa ili mtu usiweze kuwagundua na pia walikuwa wanatembea na matunguli wakiamini hawakamatwi lakini wajue Serikali hailogwi hata siku moja na tunaendelea kumtafuta mganga wao wa kienyeji,”amesema Mambosasa.
Mambosasa amesema vitu vingine walivyokamata ni kitambulisho cha kugushi chenye nembo ya polisi chenye jina la Martin Pumba simu za mkononi, silaha ikiwamo panga, nondo sime na maganda matatu ya risasi yanayodhaniwa kuwa ni ya bunduki aina ya SMG.
Amesema jeshi la polisi kanda hiyo linaendelea na mahojiano na watuhumiwa ili kubaini wanaoshirikiana nao na watafikishwa mahakamani ili kujibu tuhuma zinazowakabili.
Wakati huo huo aliwaagiza makamanda wa polisi mikoa mitatu ya jiji la Dar es Salaam waimarishe doria ili kuhakikisha wananchi wake wanakuwa salama.
Hayo yamekuja baada ya wananchi wa eneo la Mabibo na Mtongani wakiwalalamika askari polisi wa eneo husika kutochukua hatua ya kuwakamata vibaka wanaoiba maeneo hayo.
Mambosasa amesema atafuatilia maeneo yaliyolalamikiwa na wananchi hao na atakapobaini kuna uzembe atawachukulia hatua za kisheria askari polisi wa eneo husika.