WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola ameapa atapambana na baadhi ya polisi nchini ambao wanatabia ya kubambikizia kesi wananchi kwa kuwa wanaichafua Wizara yake pamoja na nchi kwa ujumla.
Katika kulifanikisha hilo, Lugola amesema atafanya ziara ya kushtukiza katika vituo vya polisi mbalimbali nchini ili kupambana na polisi wenye tabia hiyo mbaya na endapo akiwakamata hata waonea huruma.
Waziri Lugola ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mwibara, aliyasema hayo wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara na wananchi wa Kijiji cha Kenkombyo, Kata ya Neruma, jimboni kwake, wilayani Bunda, alisema tabia hiyo ya baadhi ya polisi wanayoiendeleza katika vituo vya polisi yapaswa kulaani na atakua mkali zaidi katika kulifuatilia hilo.
“Nilishawaambia polisi na leo nawaaambia tena, nitakua nafanya ziara ya kushtukiza mara kwa mara katika vituo vya polisi, na hamjui saa wala siku lini nitakuja, hili nilisemalo sitanii kabisa, lazima nitapambana nanyi, hii ni serikali ya awamo ya tano inataka wananchi waishi kwa amani zaidi bila kua na hofu ya aina yoyote,” alisema Lugola.
Lugola aliongeza kua, yeye ni mtetezi wa polisi na anajua kazi nzuri ambayo inafanywa na idadi kubwa ya polisi, lakini wale polisi wachache wenye tabia hiyo hata waonea huruma kamwe wakati analitelekeza hilo.
“Nitatetea wafanyakazi wa Magereza, Zimamoto, Uhamiaji, Polisi na wengineo wanaofanya kazi vizuri kwa kuzingatia sheria, lakini kwa wale wanaokula rushwa na kubambikiza kesi hao watapata tabu sana na hili nalisisitiza kuwa hawatapona,” alisema Lugola.
Pia aliwataka wananchi waache tabia ya kwenda kufungua kesi polisi ili kumkomoa mtu fulani kwa kua anachuki nae, na hilo likibainika huyo mwananchi mwenye tabia hiyo ambaye anashirikiana na polisi ili tu kumkomoa mtu fulani, hakika polisi na huyo mwaanchi atapambana nao.
Aliongeza kua, anataarifa baadhi ya askari wa usalama barabarani sehemu mbalimbali nchini sio tu katika Jimbo lake la Mwibara, baadhi ya askari hao wanachukua rushwa kwa wananchi ambao hawajafanya kosa lolote ila uwalazimisha ili tuu waweze kupata rushwa, hilo nalo atapambana nalo.
“Hao askari wa barabarani wakati mwingine wanawasumbua wenye magari, wakati mwingine unakuta mtu kaegesha pikipiki yake wanaichukua wanaipeleka kituoni, ukiuliza unaambiwa utaikuta kituoni, na ukienda kituoni wanakuweka ndani, na ukitoka unaombwa rushwa, mimi Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, sitarajii hilo kutokea,” alisema Lugola.
Aidha, Lugola alizungumzia kuhusu maendeleo ya jimbo lake akiwataka wananchi wa jimboni humo, licha ya kuwa wanapata fedha za maendeleo lakini wananchi hao wanapaswa kuweka nguvu katika miradi ya maendeleo katika katika sekta ya elimu, afya, kilimo pamoja na zinginezo.
Pia alisema wanatarajia kujenga kituo kikubwa cha polisi eneo la Kibara hivyo watahitaji nguvu ya wananchi katika kulifanikisha hilo kwa eneo hilo ili maendeleo yazidi kupatikana wananchi wakifanya kazi kwa amani na utulivu.
Lugola ambaye yupo ziarani jimboni kwake, licha ya kuzungumzia masuala hayo ya maendeleo, pia anafuatilia mechi za mpira wa miguu katika kata mbalimbali ndani ya jimbo hilo baada ya kuanzisha mashindano ya michezo ya Kangi Bonanza, ambapo timu mbalimbali ushiriki nawashindi upewa fedha na wachezaji bora wanasafirishwa jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuchujwa katika timu ndogo ya Klabu ya Simba, jijini humo, akiwa na lengo ya kukuza vipaji vya wananchi wake ndani ya Jimbo lake.