Waziri Mkuu Aagiza Mhasibu Aliyehamishwa Arudishwe


Na Tiganya Vincent
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa ameuagiza uongozi wa Manispaa ya Tabora kumrejesha kwenye nafasi yake ya Uhasibu Halima Temihaga ambaye alihamishiwa Ofisi ya masoko baada ya kuwalalmikia  viongozi wa Idara yake.

Mhe. Majaliwa ametoa agizo hilo leo mjini hapa wakati akizungumza na watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, wa Manispaa , Madiwani na viongozi mbalimbali ikiwa ni siku ya mwisho ya ziara yake mkoani Tabora.

Aliutaka uongozi wa Manispaa ya Tabora kumrejesha kwenye nafasi yake na  kutombugudhi mtumishi huyo.

Katika kuhakikisha agizo hilo linatekelezwa amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa huo Msalika Makungu kufuatilia kwa karibu Ofisi ya Idara ya Fedha ya Manispaa hiyo kuona utendaji kazi wake.

Waziri Mkuu alisema kuwa Halima alipewa uhamisho na Mkuu wake wa Idara baada ya kulalamikia kitendo cha kutumia namba yake ya siri kuidhinisha malipo bila ya kumshirikisha yeye mwenyewe kama Mhasibu.

Mhe. Majaliwa aliongeza kuwa katika tukio hilo hati ya malipo namba hati iliyotumika kutoa kiasi cha zaidi ya shilingi milioni tano ambazo ilidaiwa ni malipo ya kazi za ziada kwa ajili ya Wahasibu wa Manispaa hiyo ( PV  namba 2018 002321 ) ya tarehe 13 Aprili mwaka huu.

Aliongeza kuwa fedha nyingine kiasi cha shilingi  milioni 8.4 zilizotolewa kwa PV namba 2018 0001492 haijulikana matumizi yake.

Kutokana na kasoro hizo Waziri Mkuu alimtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Manispa hiyo kuwa makini na kazi yake huku akiwaagiza Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa kuisimamia kwa karibu Ofisi hiyo.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad