Ameyasema hayo leo (Jumatatu, Agosti 13, 2018) wakati akifungua kozi ya tano ya muda mfupi ya viongozi inayofanyika katika Chuo cha Taifa cha Ulinzi, Kunduchi jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu amesema chuo hicho kilianzishwa kwa lengo la kulisaidia Taifa kujenga uwezo wa viongozi ili wanaohitimu mafunzo hayo wawe na uchambuzi wa kina na wa kimkakati ili kuweza kutatua mambo mbalimbali ya usalama wa Taifa na matatizo yanayotakiwa kushughulikiwa kimkakati.
“Chuo hiki kilianzishwa ili kuwaleta washiriki kutoka taasisi zote za Serikali na sekta binafsi waweze kujadili mambo mbalimbali ya kimkakati ili wanapokuwa wanatekeleza wajibu wao watambue kuwa ni kwa kiasi gani matokeo ya maamuzi yao yataathiri mambo ya kijamii, kiuchumi, uhusiano wa kidiplomasia na siasa za ndani kwa ujumla wake”.
Amesema ushirikiano kuhusu kutatua matatizo uanze wakati wa mafunzo hayo na uendelee hata hapo baadaye watakaporejea kwenye maeneo yao ya kazi. “Sisi viongozi wenu tunatarajia kuona kuwa mtakapohitimu mafunzo haya mtakuwa mmebadilika kimtizamo na kwamba taasisi zenu zitakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuzungumza lugha moja”.
Waziri Mkuu amesema suala hilo ni muhimu sana katika kusukuma maendeleo ya nchi kwa haraka hususan wakati huu ambao Serikali inalenga kukuza uchumi wa viwanda, ambapo amewataka viongozi hao watambue kwamba changamoto za sasa ni mtambuka na hivyo, si rahisi kutatuliwa na taasisi moja moja.
“Changamoto hizi zimebadili hali ya nchi yetu ikiwa ni pamoja na uharibifu wa mazingira, ongezeko la watu, uhaba wa ajira, makosa ya kimtandao, ugaidi, na mengine mengi ambayo yote zinahitaji mikakati ya pamoja ili kuweza kukabiliana nayo”.
Awali, Mkuu wa chuo hicho Luteni Jenerali, Paul amesema mafunzo hayo yanayoanza leo Agosti 13 yanatarajia kuisha Agosti 17, ambapo mafunzo hayo yamelenga kuwanoa na kuwawezesha washiriki kujua mambo ya Usalama wa Taifa na uzalendo kwa nchi.
Pia watajifunza namna ya kuendesha Serikali kwa kutumia mikakati mbalimbali pasipo kuathiri usalama pamoja na kupata uzoefu katika mambo mbalimbali na kuwafanya wawe na uwezo wa kutengeneza, kuendeleza na kusimamia utekelezaji wa mikakati inayolenga kujenga na kuimarisha Usalama wa Taifa.