Siku chache baada ya mkuu wa wilaya ya Kisarawe Mkoani Pwani, Jokate Mwegelo kufanya oparesheni ya kukata mifugo katika maeneo ya hifadhi zilizopo wilayani humo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina amepiga marufuku tabia ya ukamataji mifugo kiholela.
Mpina ametoa marufuku hiyo wakati akifunga maonesho ya 25 ya Nane nane Kanda ya Mashariki inayojumuisha mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Pwani na Morogoro katika viwanja vya Mwalimu JK Nyerere mjini Morogoro.
Luhaga Mpina amepiga marufuku tabia hiyo ambayo imekuwa ikifanywa na baadhi ya watumishi wa umma na kusababisha mifugo mingi kufia mikononi mwa Serikali kwa kukosa huduma muhimu ikiwemo maji, malisho na matibabu hivyo kusababisha hasara kubwa kwa wafugaji na Taifa.
Mpina amesema kuwa oparesheni hizo zinapofanyika ni lazima zihusishe pia maofisa wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi ili kuwa na uelewa wa pamoja wa jambo hilo na kuepusha mifugo hiyo kuteketea kwa kukosa huduma muhimu jambo ambalo ni kinyume na haki za wanyama.
Aidha Mpina amefafanua kuwa utaratibu unaofanyika hivi sasa wa kukamata mifugo hovyo ni ukiukwaji wa sheria namba 17 ya Magonjwa ya Wanyama ya mwaka 2003 na, Sheria ya Ustawi wa Wanyama Namba 19 ya Mwaka 2008 ambazo zinataka mifugo inapokamatwa kuzingatia masuala ya magonjwa na ustawi wa mifugo katika kipindi chote inapokuwa imeshikiliwa.