Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe amesema serikali imepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha msanii nguli wa filamu nchini Bw. Amri Athumani maarufu kama King Majuto kilichotokea jana usiku katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam.
Dkt. Mwakyembe amesema hayo leo Agosti 09, 2018 katika taarifa yake iliyotolewa na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Lorietha Laurence na kusema kwamba amepokea salamu za rambirambi kutoka kwa Rais Dkt. John Magufuli kuondokewa na msanii huyo mkongwe katika tasnia ya filamu nchini
"Serikali imekuwa ikishirikiana kwa ukaribu na familia ya King Majuto tangu wakati wa kumuuguza na kumpeleka nchini India kupata matibabu zaidi. Tutaendelea kuwa karibu na familia yake katika kipindi hiki kigumu cha msiba", amesema Mwakyembe.
Marehemu King Majuto alianza kazi ya uigizaji zaidi ya miongo minne iliyopita hadi anafikwa na mauti King Majuto alikuwa akiendelea na kazi yake katika tasnia ya filamu.
Alhaji Amri Athuman alifariki Jumatano ya Agosti 8, 2018 majira ya saa 1:30 usiku katika hospitali ya taifa ya Muhimbili ambako alilazwa tangu Julai 31, 2018 kwa ajili ya kupatiwa matibabu kutokana na maradhi ambayo yalikuwa yakimsibu enzi za uhai wake.
Mwili wa marehemu Alhaji Amri Athumani kwa sasa upo Msikiti wa Maamur, ulioko Upanga jijini Dar Es Salaam kwa ajili ya kufanyiwa ibada fupi ya kusaliwa sala yake ya mwisho kabla ya kupelekwa kuagwa na umati wa wananchi katika viwanja vya Karimjee na kisha kusafirishwa Mkoani Tanga kwa maziko ambayo yamepangwa kufanyika kesho.