Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Hussein Mwinyi, amewataka Waislam na Watanzania kwa ujumla kuendelea kudumisha amani ya nchi kwa maendeleo ya taifa.
Akizungumza leo Jijini Dar es Salaam, kwenye Baraza la Eid, Dkt. Hussein Mwinyi, amesema serikali ya awamu ya tano imejikita katika kuwaletea maendeleo wananchi hivyo jambo hilo halitawezekana pasipo kuwa na amani.
Aidha ameongeza kuwa Amani ndio msingi wa kila kitu katika nchi yoyote ili watu waweze kufanya shughuli zao za kila siku ikiwemo ibada na kusema Mwenyezi Mungu ameitunuku Tanzania kuwa nchi ya amani hivyo Watanzania hawana budi kuitunza na kuilinda amani nchini.
Katika hatua nyingine Dkt. Mwinyi, amelipongeza Baraza la Waislam Tanzania (BAKWATA), kwa kujitathmini katika utendaji wake wa kazi kwa faida ya Waislam wote ikiwemo kuanza kujihusisha na utoaji wa huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo Elimu na Afya.
Kwa upande wao viongozi wa dini ya kiislam waliopata nafasi ya kutoa hotuba kwenye Ibada hiyo ya Eid wamewataka wananchi kuunga mkono juhudi za serikali katika kuinua uchumi wa nchi kupitia viwanda lakini pia kuendelea kudumisha na kuilinda Amani iliyopo.