Waziri wa Áfya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mh. Ummy Mwalimu leo amefanya ziara katika mpaka wa Rusumo kati ya nchi ya Tanzania na Rwanda ili kuangalia ni jinsi gani mkoa wa Kagera umejipanga katika kudhibiti ugonjwa wa Ebola kuingia nchini.
Waziri wa Áfya Ummy Mwalimu kushoto, akitoa maelekezo kwa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera Dkt Marco Mbata kulia.
Akiwa mpakani hapo Waziri Ummy amesema kuwa mlipuko wa ugonjwa wa Ebola ambao umetokea eneo la Kivu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo unaiweka Tanzania katika hatari zaidi ya kuweza kupata wagonjwa wa Ebola kutokana na muingiliano wa wananchi baina ya nchi hizo.
Aidha, amebainisha kuwa Serikali inaendelea kutoa mafunzo kwa wahudumu wa Sekta ya Áfya ili kufahamu jinsi ya kuwahudumia wanaohisiwa kuwa na virusi vya ugonjwa wa Ebola sambamba na hilo Serikali imeleta vifaa kinga watakavyovaa wakati wakitoa huduma kwa mgonjwa au mhisiwa wa ugonjwa wa Ebola.
Hata hivyo Mh. Ummy ameweka wazi kuwa serikali inaendelea kuweka mikakati thabiti katika maeneo yote hatarishi ikiwemo kufanya udhibiti mipakani na njia za panya ili kuhakikisha hakuna mtu anaingia na ugonjwa wa Ebola nchini.
Ebola imeripotiwa kutokea nchini DR Congo eneo la Kivu Kaskazini ambalo ni karibu na Tanzania hivyo hofu imekuwa kubwa kwa ugonjwa huo kufika nchini kutoka na muingiliano wa wananchi baina ya nchi hizi mbili.