Zari Kiboko! Amfanyia Umafia Daimond Kwenye Birthday ya Tifa

Zari Kiboko! Amfanyia Umafia Daimond Kwenye Birthday ya Tifa
NI umafia wa ajabu! Hakuna maneno mengine mazuri unayoweza kuyazungumza kusherehesha tukio la mwanamama wa Kiganda, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’ alilomfanyia mzazi mwenzake, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ katika sherehe ya bethidei ya mtoto wao, Latifah Nasibu ‘Tiffah Dangote’ iliyokuwa ifanyike Agosti 17, mwaka huu huko Afrika Kusini ‘Sauz’, Ijumaa Wikienda lina ‘full’ stori.



Awali, Diamond alijinasibu kuangusha bonge la sherehe nchini humo na kutangaza mbwembwe kibao zikiwemo za kuwasafirisha watoto 10 sambamba na wazazi wao kutoka Bongo hadi Sauz pamoja na ile kamati ya sherehe iliyofanikisha sherehe ya 40 ya mtoto wa mtangazaji Zamaradi Mketema.



TUPATE HABARI KAMILI

Katika ‘kufukunyua’ ukweli wa mambo katika bethidei hiyo ya ‘taifa’, Ijumaa Wikienda lilifanikiwa kuzungumza na mtu wa ndani ambaye alilieleza jinsi Zari alivyomfanyia umafia Diamond kiasi cha kumfanya jamaa huyo anyooshe mikono na kuahirisha sherehe hiyo bila kupenda.



“Unajua ile bethide Diamond alikuwa anaiandaa kwa ushirikiano na kampuni (anaitaja jina) na kampuni hii ndiyo ambayo inawadhamini Diamond na Zari katika mambo mbalimbali kwani kampuni hiyo nayo inanufaika pia kwa jinsi wawili hao wanavyoitangaza kupitia matangazo mbalimbali wanayoyaandaa. Sasa kulikuwepo makubaliano kwamba ili wadhamini hao waendelee kutoa fedha, Diamond na Zari wanapaswa kuposti sherehe hiyo katika akaunti zao za Instagram, sasa mwanzoni bidada Zari anaonekana alikubali, lakini kadiri siku zilivyokuwa zinaenda akapiga kimya tu,” kilisema chanzo hicho cha ndani.


CHAZIDI KUTIRIRIKA

Chanzo hicho cha ndani kilizidi kutiririka kuwa, kutokana na uzito wa tukio hilo, Diamond alifanya jitihada za makusudi za kumshawishi Zari ili aposti tukio hilo ili wadhamini waone, lakini mwanamama huyo mwenye makazi yake pande za Sauz alikuwa ni kama vile ameweka pamba masikioni, hakumsikiliza wala kukubaliana naye chochote.



“Yaani Zari alimlia bati ileile, hata baada ya kumueleza namna ambavyo kampuni imekubali kuwasafirisha watu na wazazi wao na kwamba hata yeye binafsi ameandaa kitu kikubwa, lakini Zari ilikuwa ni kama linaingilia huku na kutokea kule.



APOSTI MAMBO YAKE

“Kuonesha kwamba amedhamiria kumpotezea, hadi siku zilipokaribia, Zari alikuwa bize kuposti vitu vyake ikiwemo ishu ya Miss Uganda ambayo Zari alikuwa mmoja wa majaji,” kilisema chanzo hicho. Aidha, chanzo hicho kilisema, mbali na Zari kuposti Miss Uganda, aliendelendelea kumfungia vioo Diamond kwa kuposti masuala yake mengine yakiwemo ya kutoa misaada mashuleni.



SIKU YA TUKIO

Ijumaa iliyopita ambayo ndiyo ilikuwa siku ya tukio, Ijumaa Wikienda lilizungumza na chanzo hicho cha ndani ambacho kilieleza kuwa, Diamond ameshasalimu amri na kuamua kumuachia Mungu. “Diamond ameishiwa pozi kabisa maana hata ule mchakato wa wale watoto aliouanzisha kwenye ukurasa wake wa Instagram, ameshindwa hata kutoa hatma yake.



“Ile kamati aliyoinadi siku ya 40 ya mtoto wa Zamaradi iliyokuwa na mastaa amekosa kabisa cha kuwaambia na kuamua kukaa kimya tu na wenyewe pia kwa aibu wameinamisha vichwa vyao maana hawana jinsi ya kufanya,” kilieleza chanzo hicho.



DIAMOND ANASEMAJE?

Juzi Jumamosi baada ya sherehe hiyo kutofanyika, Ijumaa Wikienda lilijaribu kumtafuta Diamond ili kumsikia anazungumziaje ishu hiyo, hata hivyo, simu yake iliita bila kupokelewa.



MAMA DIAMOND, TALE AIBU YAO

Pamoja na Ijumaa Wikienda kupata ubuyu wa sherehe hiyo kubuma muda mrefu, hadi inafika siku moja kabla ya sherehe, mama mzazi wa Diamond, Sanura Kassim ‘Sandra’ na meneja wa Diamond, Hamis Taletale ‘Babu Tale’ walinukuliwa wakisisitiza sherehe hiyo ipo na wanaenda Sauz kama kawaida.



“Unajua hii ni pati, bethidei ya Tiffah ilishapita lakini nikwambie tu itafanyika na kutakuwa na sapraizi mtaona,” alinukuliwa Tale katika gazeti la Ijumaa la wiki iliyopita lililokuwa na kichwa cha habari kilichosomeka; MOND, ZARI CHUMBA KIMOJA SAUZ.



MAMA DIAMOND

“Wewe ukitaka kuniuliza kuhusu safari nitakujibu tu ipo palepale, lakini hayo mambo yenu mengine ya kidaku mimi siwezi kuyajibu.”



GLOBAL ISHAJUA KITAMBO

Kabla ya mama Diamond na Tale kuaminisha Watanzania kuwa safari ya Sauz ipo palepale hali ilioliaminisha Gazeti la Ijumaa kuandika habari ya kuwa Diamond na Zari watalala pamoja Sauz, gazeti hilo pamoja na mengine ya Global yalishaandika kutilia shaka uwezekano wa sherehe hiyo kufanyika.

Kwenye gazeti la Amani la Julai 26, mwaka huu toleo namba 1032 lilikuwa na kichwa cha habari kilichosomeka; UTATA WAIBUKA BETHIDEI YA TIFAH.



Kwenye habari hiyo, Amani lilijiridhisha kwa asilimia 90 kwamba sherehe hiyo haiwezi kufanyika kutokana na kuhakikishiwa na watu wa karibu na Zari kuwa haitakuwepo na mrembo huyo ameamua kumpotezea Diamond na washirika wake.



TUJIKUMBUSHE

Kumbukumbu inaonesha kwa kawaida, bethidei ya Tiffah aliyezaliwa mwaka 2015 ni Agosti 6, lakini mwaka huu Diamond aliamua kuisogeza mbele hadi Agosti 17 ili aweze kumaliza ziara yake ya kimuziki nchini Marekani.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad