Ashambuliwa kwa Kupigwa Viboko Baada ya Kumnywesha Pombe Kali Mtoto wa Miezi Minanae

Ashambuliwa kwa Kupigwa Viboko Baada ya Kumnywesha Pombe Kali Mtoto wa Miezi Minanae
MKAZI wa Kijiji cha Buzirayombo wilayani Chato, mkoani Geita, Makubi Wanjala (25) amecharazwa viboko vitano kwenye makalio baada ya kubainika kumpa pombe kali mtoto wa miezi minane.

Kijana huyo ambaye ni mvuvi wa samaki kwenye mwalo wa Chato Beach, alikutana na kichapo hicho jana, majira ya saa tatu asubuhi eneo la mwalo huo baada ya kuomba kumbeba mtoto huyo kabla ya kumnywesha pombe kali aina ya "Shimha".

Akizungumza na gazeti hili, Mwenyekiti wa kitongoji cha Kalema, Fares Kabunazi, alisema akiwa kwenye majukumu yake ya kawaida alipokea simu kutoka kwa mmoja wa wavuvi kuwa anahitajika haraka eneo la mwalo wa Chato Beach na kuelezwa kuna dharura imejitokeza eneo hilo.

Baada ya kufika eneo la tukio alimshuhudia mtoto wa miezi minane (jina tunalihifadhi) akiwa amelegea kutokana na kupewa pombe hiyo.

Kiongozi huyo alifanikiwa kunusuru maisha ya kijana huyo baada ya kuuzuia umati wa wananchi waliokuwa wamekusanyika eneo hilo wakiwa na lengo la kumdhuru kijana huyo kutokana na kitendo chake cha kumnywesha pombe mtoto mdogo.

"Kutokana na jazba walizokuwa nazo wananchi na baada ya kumsikiliza mtuhumiwa pamoja na mama mzazi wa mtoto huyo, niliamua kutoa amri ya kucharazwa viboko vitano kwenye makalio yake na kumfukuza kufanya shughuli za uvuvi kwenye mwalo huo," alisema Kabunazi.

Akisimulia mkasa huo, mama mzazi wa mtoto hiyo, Husna Ally (28), alisema kijana huyo alifika dukani kwake na kukaa kwenye moja ya viti vilivyoko eneo hilo, huku akitumia pombe kali iliyoko kwenye kifungashio cha chupa ya plastiki na kuomba kumbeba mtoto huyo.

"Alipofika hapa dukani kwangu pamoja na pombe yake aliniomba kumbeba mtoto wangu...bila kuelewa kinachoendelea, nilimpa mtoto kwa nia njema kabisa, lakini baadaye ndiyo nilishangaa kumwona akimnywesha mwanangu pombe, huku mtoto akiendelea kulegea...ndipo baadhi ya wananchi walivyoona hali hiyo wakampigia simu mwenyekiti wetu wa kitongoji," alisema Husna.

Kwa upande wake kijana huyo, Makubi Wanjala, alikiri kumnywesha mtoto huyo pombe kwa madai hakujua kama ni kosa na kudai alimpa kiasi kidogo tu cha pombe hiyo.

Hata hivyo, alisema anajutia kosa hilo kutokana na kucharazwa bakora tano kwenye makalio kwa kuwa aliamini alikuwa akiburudika baada ya kumaliza kazi ya uvuvi.

Kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 Ibara ya 13 kifungu kidogo cha (1), mtu yeyote haruhusiwi kumtesa mtoto au kumfanyia vitendo vingine vya ukatili, kumpa adhabu za kinyama au kumdhalilisha ikiwa ni pamoja na kumfanyia mambo ya kimila yanayoondoa utu wake au yenye madhara katika ustawi wake kimwili au kiakili.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad