Jeshi la polisi mkoni Tabora linawashikilia askari wake 10 kwa kusababisha kifo cha Selemani Jumapili ambaye alifariki muda mfupi baada ya kufikishwa katika hospitali ya wilaya Igunga kwa matibabu..BABA wa kijana aliyeuawa kwa kupigwa na Polisi tisa wilayani Igunga, mkoani Tabora, Selemani Jumapili (22), Jumapili Juma, ameelezea namna mwanawe alivyokamatwa, kupigwa na kuteswa na askari hao hadi kupoteza maisha.
Baba huyo ameyasema hayo juzi katika maziko ya kijana hiyo yaliyohudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri pamoja na Kamanda wa Polisi mkoa wa Tabora, Emmanuel Nley. Amesema siku ya tukio akiwa kazini muda wa saa 11 jioni alipigiwa simu na baadhi ya wananchi kuwa mwanawe amekamatwa na polisi huku wakimwambia kuwa amepigwa vibaya baada ya kukamatwa.
Amesema baada ya kumaliza kupokea ujumbe huo alikwenda hadi kituo cha polisi Igunga ambako alikuta mwanawe amewekwa mahabusu na alipoomba amwekee dhamana askari waliokuwa zamu walimkatalia huku wakimtishia kumweka mahabusu. Alisema kutokana na vitisho alivyotolewa na askari hao, aliamua kurudi nyumbani na ilipofika saa tano usiku baadhi ya raia wema walimpigia simu wakimtaarifu kuwa mwanawe amelazwa hospitali ya wilaya, wodi namba nane akiwa chini ya uangalizi wa askari huku akiwa na pingu mikono yote.
Amesema baada ya ujumbe huo alikwenda usiku huo huo hadi hospitali ya wilaya ya Igunga ambako alimkuta mwanawe amelazwa wodi hiyo huku akiwa amefungwa pingu mikono yote ambapo alimuomba askari amfungue pingu mkono mmoja, askari huyo aligoma na muda mfupi kijana huyo akafariki dunia. “Mwanangu Selemani ameniuma sana kwani sijui hata kosa alilofanya hadi polisi kutumia nguvu kubwa, basi mimi namuachia Mwenyezi Mungu na serikali,” alisema mzazi wa marehemu huku akibubujikwa na machozi.
Nao baadhi ya mashuhuda waliokuwepo Flora Ambikile na Aloyce Kitundu walisema askari hao baada ya kufika kwenye eneo alilokuwa akifanyia biashara ya kuchoma nyama Selemani walimuuliza kwa nini anafanya biashara kabla ya muda unaotakiwa. Walisema askari hao hawakutaka ajieleze na hatimae walianza kumshambulia kwa mateke kisha kumfunga pingu na kumtupia kwenye gari kama mzigo wa gunia la mahindi kisha kuondoka naye kituo cha polisi.
Mganga mfawidhi wa hospitali ya wilaya Igunga Merchades Magongo alikiri kumpokea Selemani muda wa saa 3 usiku wa Agosti 29 na kuongeza kuwa walimpokea akiwa na askari ambapo wakati akiendelea kumpatiwa matibabu muda wa saa tano usiku alifariki dunia. Akizungumza msibani hapo, Mkuu wa Mkoa Mwanry amewataka wananchi wa Igunga kuendelea kuwa watulivu wakati suala hilo likishughulikiwa na serikali.
Aidha, amemuagiza Kamanda wa Polisi Nley kuwakamata askari wote waliohusika na mauaji ya kijana huyo na kuongeza kuwa serikali haiko tayari kuona watu wachache wakichafua utendaji mzuri wa serikali. Mganga Mkuu wa mkoa wa Tabora, Dk Gunini Kamba na Mganga mfawidhi wa hospitali ya rufaa Kitete mkoani hapa Kelvin Nyakimori walioufanyia uchunguzi mwili wa marehemu alisema uchunguzi unaonesha kuwa kifo chake kilitokana na kupigwa na kitu kizito kwenye kisogo.
Mbunge wa Igunga, Dk Peter Dalali Kafumu ambaye ni miongoni mwa viongozi walioshiriki maziko ya kijana huyo yaliyofanyika katika makaburi ya Masanga Septemba mosi, mwaka huu, alilaani vikali kitendo hicho na kuwataka askari kufanya kazi kwa kuzingatia sheria za nchi.
Alimuomba mkuu wa mkoa Tabora Mwanri kufuatilia suala hilo kwa karibu ili haki itendeke.
Kamanda Nley alithibitisha kutokea kwa tukio hilo la kuuawa kwa mfanyabiashara wa nyama Selemani ambapo alisema hadi sasa askari tisa wanashikiliwa na jeshi hilo hata hivyo hakuwa tayari kutaja majina na vyeo vyao.
Alisema utafanyika gwaride ili kubaini waliohusika na kifo hicho kwani hakuna mtu aliyejuu ya sheria. Imamu wa msikiti mkuu wa Ijumaa wilaya ya Igunga Swalehe Hamisi alitoa mwito kwa viongozi wa serikali waliopewa dhamana ya kuwatumikia wananchi kufanya kazi kwa makini pamoja na kuwa na hofu ya Mungu kwa kutofanya mambo yanayomchukiza Mwenyezi Mungu pamoja na jamii kwa ujumla.