BAADA ya kuendelea kung’ara katika Ligi Kuu ya Ubelgiji na michuano ya Ulaya, mshambuliaji Mtanzania wa KRC Genk, Mbwana Samatta thamani yake katika soko la wachezaji imezidi kupaa na kufikia kiasi cha euro milioni 3 ambayo ni zaidi ya Sh bilioni 8.
Mapema mwanzoni mwa mwaka huu thamani ya Samatta ilikuwa ni euro 2.70m (Sh bilioni 7), huku akiwa hayupo katika kiwango kizuri kutokana na kuwa majeruhi mara kwa mara.
Samatta alijiunga na Genk msimu wa mwaka 2016 akitokea TP Mazembe ya DR Congo, amerejea kwenye kiwango cha juu, wiki chache zilizopita akafanikiwa kupiga hat trick yake ya kwanza akiwa na timu hiyo kisha akafunguka kupitia ukarasa wake wa Instagram kwa kusema:
“Nina furaha kufunga hat trick yangu ya kwanza nikiwa na Genk, nina imani nyingine nyingi zinafuata, haina kufeli.”