Msanii wa miondoko ya singeli nchini, Dullah Makabila amekanusha tetesi za yeye kujihusisha na masuala ya imani za kishirikina na kudai picha iliyokuwa inasambazwa mitandaoni ni moja ya sehemu ya kazi yake na sio vinginevyo.
Dullah Makabila ametoa ufafanuzi huo leo Septemba 25, 2018 alipokuwa anazungumza na www.eatv.tv baada ya kusambaa picha yake mitandaoni, ikimuonyesha anachanjwa chale na mganga wa kienyeji jambo ambalo watu wengi liliwashtua, huku wengine wakienda mbali zaidi kuwa muziki wa singeli ndio ulivyo wasanii wake kuegemea kwenye masuala ya kishirikina.
"Hapana mimi sifanyi masuala ya kishirikina ili kusudi muziki wangu uende mbele, ile ni picha ilipigwa kwenye maandalizi ya 'video' ya wimbo wangu mpya utakaoitwa mganga. Sio kweli kwamba muziki wa singeli unaendeshwa na 'ndumba' kama mtu hujui ni hujui tu na mambo hayo hayawezi kukubadilisha", amesema Dullah Makabila.
Pamoja na hayo, Dullah Makabila ameendelea kwa kusema kuwa "nawaomba mashabiki zangu wasijisikie vibaya kuhusiana na hiyo picha inayosambazwa mitandaoni, kwani hiyo ni moja ya sehemu ya kazi yangu na watakuja kushuhudia wenyewe maana wasije kunifikiria kuwa mimi ndio nilivyo hivyo".
Mbali na hilo, Dullah Makabila amesema kwa sasa anafurahi kuona umoja uliopo kwa wasanii wenzake wa singeli baada ya kuzivunja tofauti zao walizokuwa nazo hapo awali.
Katika miaka ya hivi karibuni, wasanii wa muziki wa singeli walikuwa wanaongoza kwa kuwekeana vinyongo katika ufanyaji wa kazi zao, kwa kujifanya kila mmoja yupo juu ya mwenzake na bora zaidi yake.
Baada ya Picha Yake Akiwa Kwa Mganga Kusambaa kwenye Mitandao Dulla Makabila Afunguka Ilivyokuwa
0
September 25, 2018
Tags